Walioshuhudia tukio hilo wameiambia sauti ya Amerika VOA kwamba shambulizi limetokea karibu na kizuizi cha usalama wakati wafanyakazi wa wizara hiyo wapolikuwa wanatoka kazini.
Msemaji wa polisi wa utawala wa Taliban Khalid Zadran, amesema kwamba maafisa watatu wa usalama ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa.
Shirika la kimataifa la misaada ya kibinadamu linalojulikana kama Emergency, limethibitisha kwamba watu 12 waliojeruhiwa walihudumiwa katika kituo cha matibabu kilichopo karibu na sehemu ya tukio.
Kati yao ni mtoto wakati watu wengine wawili walikuwa wamefariki walipofikishwa kwenye kituo hicho.
Kundi la kigaidi la Islamic State limedai kutekeleza shambulizi hilo, ambalo ni la kwanza kutokea Afghanistan tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadan.
Kundi la Islamic state Khorasan, lenye ushirikiano na kundi la Islamic state, limedai kutekeleza mashambulizi yote ambayo yametokea katika siku za karibuni nchini Afghanistan.
Shambulizi hilo limetokea baada ya Taliban, adui mkubwa wa Islamic State Khorasan, kutangaza kwamba maafisa wake wa usalama walikuwa wamewaua magaidi watatu wa IS-K, katika operesheni ya hivi karibuni katika ngome za wapiganaji hao, katika mkoa wa Balkh, kaskazini mwa Afghanistan.
Wapiganaji wa Taliban wamekuwa wakitekeleza operesheni za kila mara katika ngome za kundi la IS-K mjini Kabul na sehemu nyingine za Afghanistan na kuua makamanda wa ngazi ya juu wa kundi hilo.