Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 28, 2023 Local time: 09:13

CCTV kuwekwa miji yote ya Kenya


Mfano wa kamera zitakazowekwa katika miji ya Kenya ili kupambana na ugaidi na kuimarisha ulinzi

Wakazi wa Kenya wana mtazamo tofauti juu ya kamera za kupambana na ugaidi zinazotarajiwa kuwekwa nchini humo

Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga amesema nchi yake imepokea fedha kutoka China za kugharamia kamera za kufuatilia matukio mbalimbali nchini humo katika juhudi za kupambana na ugaidi katika miji ya Kenya.

Bwana Odinga aliliambia bunge la Kenya kuwa katika siku za karibuni serikali itaweka kamera hizo zinazojulikana kama CCTV kote nchini Kenya kuanzia jiji kuu la Nairobi ikifuatiwa na Mombasa , Kisumu na miji mingine. Alisema serikali ya Kenya imepokea msaada wa dola milioni 100 kutoka China za kupambana na ugaidi na kuimarisha ulinzi nchini humo.

Lakini katika mitaa ya Nairobi wakenya walikuwa na hisia mbalimbali. Albert Bwire alisema hiyo ni dhana nzuri ya kuweka kamera za CCTV ili kurekodi visa vya uhalifu haswa wakati wa uchaguzi. Lakini Jimmy Kariuki alipinga mpango huo akisema hadhani utasaidia chochote. Alihoji kwanini serikali inalenga miji mikubwa bila kuwafikiria wale waliopo vijijini.

Mkenya mwingine Alois Gitonga alieleza wasiwasi wake juu ya uwezekano wa ufisadi katika mradi huo. Alisema Kenya imekuwa na kashfa nyingi sana. Kwa hiyo hawezi kusema kwa uhakika kwamba mpango huu utafanikiwa ama fedha hizo hazitaishia kwenye mfuko wa mtu.

Serikali ya Kenya imeongeza juhudi zake za kupambana na ugaidi katika miaka ya karibuni ikitilia uzito zaidi jamii kubwa ya wasomali nchini humo baada ya mashambulizi kutoka Somalia kwenye mpaka wake na Somalia, utekaji nyara wa watalii , wafanyakazi wa kutoa misaada na hata askari polisi wa Kenya.


XS
SM
MD
LG