Polisi nchini Uganda wamefyatua gesi ya machozi kwa waandamanaji waliokuwa wanarusha mawe na kumkamata kwa muda kiongozi wa juu wa upinzani jumanne wakati wa kuanza tena maandamano ya kupinga ongezeko la chakula na mafuta.
Maafisa wa usalama walimkamata Kizza Besigye baada ya kuondoka nyumbani kwake nje ya mji wa Kampala kushiriki katika maandamano ya kutembea kwenda kazini . Baadae Besigye aliachiliwa na kurejeshwa nyumbani.
Waandamanaji wamekusanyika katika kitongoji cha Kasangati , karibu na nyumba ya Beigye kupambana na polisi ambao walifyatua gesi ya machozi na risasi za mpira kutawanya mkusanyiko wa watu.
Pia jumanne maafisa wa usalama walisema wafuasi wa upinzani 12 ambao walikamatwa jumapili wameshitakiwa kwa mkosa ya uhaini.
Kundi la upinzani la wanaharakati wapenda mabadiliko lilitoa mwito wa mzunguuko mpya wa maandamano ya kutembea kwenda kazini wiki hii licha ya Serikali kutoa onyo dhidi ya maandamano kama hayo. Maafisa wa usalama walitumia nguvu kusitisha maandamano kama hayo mwezi Aprili na Mei.