Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Septemba 26, 2022 Local time: 16:43

AU yataka ICC iahirishe kesi za viongozi wa Kenya


Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika Addis Ababa, Ethiopia Oct. 11, 2013.
Viongozi wa Umoja wa Afrika wanaokutana mjini Addis Ababa,Ethiopia wametoa mwito wa kuahirishwa kwa kesi dhidi ya viongozi wa Kenya, zinazoendeshwa na mahakama ya kimataifa – ICC.

Katika mkutano wao Jumamosi wakuu wa nchi za Afrika walieleza kutoridhika kwao na mahakama hiyo ya The Hague, wakisema imekuwa ikiwabagua na kuwalenga waafrika.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, aliisihi mahakama ya ICC kuwa sikivu kwa maswala yaliyoibua wasiwasi miongoni mwa nchi 54 wanachama wa Umoja wa Afrika.

Desalegn alisema ni vyema ifahamike kuwa lengo la Waafrika sio kampeni dhidi ya ICC, bali mwito wa unyenyekevu kwa mahakama hiyo kusikiliza kwa makini wasiwasi na maombi ya bara la Afrika.

Aidha Waziri Mkuu Desalegn alisema kesi zinazoendelea mahakamani humo zinazuia viongozi wa Kenya kushughulikia maswala muhimu ya nchi yao. Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anakabiliwa na kesi katika mahakama hiyo Novemba 12 ambapo inadaiwa alihusika katika uchochezi wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 na mapema 2008.

Naibu rais wa Kenya William Ruto pia anakabiliwa na mashtaka sawa na hayo. Rais wa Sudan Omar al-Bashir ambaye pia amehudhuria mkutano huo wa umoja wa Afrika huko Addis Ababa anakabiliwa na mashtaka katika mahakama hiyo kwa uhalifu dhidi ya binadamu katika mkoa wa Darfur magharibi mwa Sudan.

Miongoni mwa kesi nyingine mbele ya mahakama hiyo ya ICC zinazotegemewa kusikilizwa karibuni ni ile ya rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo. Anashtakiwa kwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu.
XS
SM
MD
LG