Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton amelazwa katika hospitali moja ya mjini New York baada ya kufanyiwa operesheni kuboresha upitaji wa damu katika moyo wake. Kulingana na mshauri wake wa maswala ya sheria, Douglas Band, rais huyo wa zamani alikwenda hospitali ya
Columbia Presbeyterian baada ya "kujisikia maumivu katika kifua."
Taarifa hiyo imesema Bw Clinton, mwenye umri wa miaka 63, alikwenda kumwona daktari wake wa moyo na kufanyiwa operesheni hiyo ndogo ambayo ilikuwa ni pamoja na kuweka nyaya mbili ndogo kufungua mishipa ya moyo wake.
Band alisema katika taarifa hiyo kuwa rais huyo wa zamani yuko katika hali nzuri na "ucheshi" na ataendelea na kazi zake za taasisi yake pamoja na wadhifa wake kama mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika juhudi za misaada Haiti. Bw Clinto alikuwa Haiti kwa mara ya pili katika muda wa chini ya wiki moja mwezi uliopita.
Alhamisi jioni mkewe Clinton, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton alionekana akiingia katika hospitali hiyo kuwa na mumewe.