Ugonjwa huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza tarehe 20 Januari 2025 katika Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera ambapo watu wawili kutoka mkoani humo walithibitika kuwa na maambukizi na kupoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu.
Katika ripoti iliyotolewa na Waziri wa Afya Jenista Mhagama imeeleza kuwa mgonjwa wa kwanza aliripotiwa tarehe 28 Januari 2025 na ambapo tarehe 1 mwezi Machi 2025 siku 42 zilikamilika bila ya kuwa na maambukizi mapya, na hivyo kukidhi vigezo vya shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kumalizika kwa mlipuko huo wa Marburg.
“Kitaalamu na kulingana na kanuni na taratibu za Shirika la Afya Duniani WHO, tumekidhi vigezo vya kutangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa Marburg. Hivyo basi, leo tarehe 13 Machi, 2025, ninatangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa Marburg nchini.” Amesema Mhagama.
Wataalamu wa Afya nchini Tanzania wanasema licha ya kumalizika kwa ugonjwa huo, serikali inapaswa kuboresha utoaji wa taarifa pindi kunapotokea magonjwa ya mlipuko kutokana na taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo huchelewa kutolewa na mamlaka husika.
Daktari wa Afya Betty Sanga kutoka Dar es Salaam anasema serikali inapaswa kuongeza juhudi za utoaji wa taarifa za elimu juu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko pindi yanapojitokeza.
“Juhudi za kusambaza taarifa za kuelimisha watu jinsi ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko bado hazitoshi, kwahiyo kuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu kama taifa ili kuweza kupambana na haya magonjwa ya mlipuko” Amesema Sanga.
Waziri wa Afya pia amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo licha ya kutangazwa kumalizika ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, pamoja na kutoa taarifa za uvumi au tukio lolote lisilo la kawaida katika jamii.
Dkt Mugisha Ntiyonza rais wa Chama cha Madaktari Tanzania amepongeza jitihada zilizofanywa na wizara ya Afya, jamii, madaktari na vyombo vya kimataifa katika kupambana na kuhakikisha Tanzania inakabiliana na ugonjwa huo.
“Ni hatua muhimu sana na ya kupongezwa katika sekta ya Afya Tanzania watu wote walioshiriki wataalamu, Madaktari, watoa huduma, wananchi wa mkoa wa Kagera Jumuiya za kimataifa (WHO) na wengine wote walioshiriki katika mapambano haya pongezi sana” amesema Dkt Ntiyonza.
Aidha, Dkt Ntiyonza ameitaka serikali kuendelea kuboresha mifumo ya udhibiti na utambuzi ili kuweza kuhakikisha kuwa nchi ya Tanzania inaendelea kuwa salama wakati wote.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika.
Forum