Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 05:26

Waziri Mkuu wa Mali ajiuzulu


Waziri Mkuu wa zamani wa Mali, Cheikh Modibo Diarra akiwa Bamako, August 10, 2012.
Waziri Mkuu wa zamani wa Mali, Cheikh Modibo Diarra akiwa Bamako, August 10, 2012.
Waziri Mkuu wa muda nchini Mali Cheikh Modibo Diarra amejiuzulu saa kadhaa baada ya kukamatwa na wanajeshi wakati alipokuwa akijiandaa kuondoka nchini humo.

Bwana Diarra hakutoa maelezo yeyote juu ya kujiuzulu kwake wakati alipotoa taarifa fupi kwa njia ya televisheni mapema Jumanne. Aliwaomba msamaha raia wa Mali akisema walitaabika kutokana na matatizo ya uongozi. Alisema yeye na serikali yake walijiuzulu kwa maslahi ya amani.

Baadae msemaji wa jeshi Bakary Mariko aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba bwana Diarra ilibidi aondoke kwa sababu alikuwa anazizuia taasisi. Pia alisema bwana Diarra na Rais wa muda Diouncounda Traore walikuwa hawakubaliani katika kila jambo.

Umoja wa Ulaya-EU unasema mipango yake ya kupeleka tume ya kijeshi ya mafunzo nchini Mali itaendelea lakini EU iliisihi serikali ya muda ya nchi hiyo kumteuwa Waziri Mkuu mpya haraka iwezekanavyo. Msemaji wa mkuu wa masuala ya mambo ya nje Catherine Ashton alisema EU inafuatilia kwa karibu hali nchini Mali.

Wanajeshi wapatao 250 wa EU wanatarajiwa kupelekwa nchini Mali kutoa mafunzo kwa wanajeshi huko na kusaidia kuliimarisha jeshi dhaifu la nchi hiyo. Juhudi hizo zinamaanisha kuisaidia serikali kupata tena udhibiti wa upande wa kaskazini ambako wanamgambo wa ki-Islam wanadhibiti eneo hilo kwa sasa.

Mivutano nchini mali iliongezeka katika wiki za karibuni katika serikali ya umoja, inayomjumuisha bwana Diarra, Rais na Kapteni Amadou Sanogo ambaye aliongoza mapinduzi ya kijeshi huko Mali mwanzoni mwa mwaka huu. Mwezi Agosti nchi hiyo iliunda serikali ya kushirikiana madaraka chini ya uongozi wa bwana Diarra.

Waziri Mkuu wa zamani yupo katika kizuizi cha nyumbani katika eneo lisilojulikana.
XS
SM
MD
LG