Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 05:55

AU yataka Kiir, Machar wasiwe kwenye serikali mpya ya Sudan Kusini


Rais Salva Kiir (L) na kiongozi wa waasi Riek Machar
Rais Salva Kiir (L) na kiongozi wa waasi Riek Machar

Mazungumzo ya amani yaliakhirishwa kwa muda usiojulikana mjini Addis Ababa Ijumaa kutokana na tofauti baina ya pande hizo mbili.

Ripoti iliyovuja kutoka Umoja wa Afrika-AU inatoa wito kwa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na mpinzani wake mkuu Riek Machar kutoingia katika serikali ya mpito na kwamba nchi hiyo iliyopo kwenye mzozo wa vita iwekwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Afrika.

Shirika la habari la Uingereza-Reuters lilisambaza maelezo ya ripoti ya Ijumaa huku mzunguko mwingine wa mazungumzo kuelekea kumaliza miezi 15 ya mgogoro wa Sudan Kusini uliomalizika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia bila ya kufikiwa mkataba wa amani.

Kulingana na ripoti ya Reuters, Rais Salva Kiir na Makamu Rais wake wa zamani ambaye aligeuka kuwa kiongozi wa waasi Riek Machar wanatakiwa kupigwa marufuku wasiwe katika majukumu katika “bodi ya utendaji ya serikali ya mpito” pamoja na mawaziri wote waliopo madarakani kabla ya baraza la mawaziri kuvunjwa hapo Julai mwaka 2013.

Ripoti hiyo inapendekeza kuudwa kwa jopo litakaloteuliwa na Umoja wa Afrika na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa ili kuangalia kipindi cha miaka mitano ya serikali ya mpito nchini Sudan Kusini. Mapato ya mafuta yatakwenda kwenye akaunti ya Escrow itakayoangaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Reuters inasema ripoti ya AU pia inatoa wito wa kuundwa kwa jeshi la walinda Amani wa Umoja wa Afrika linaloundwa na wanajeshi “ wasio husishwa awali au wenye masilahi ya moja kwa moja na Sudan Kusini”.

Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka serikali ya Sudan Kusini. Msemaji wa waasi mjini Addis Ababa, Puet Kang Chol, alitaka ripoti nzima kutangazwa.

Watu waliokoseshwa makazi Sudan Kusini kufuatia mapigano yanayoendelea
Watu waliokoseshwa makazi Sudan Kusini kufuatia mapigano yanayoendelea

Mapigano yalizuka tena nchini Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka 2013 miezi sita baada ya Rais Kiir kumfuta kazi bwana Machar kama Makamu Rais. Mapigano hayo yamechochea migawanyiko ya kikabila nchini humo ambako kabila la Dinka linamuunga mkono Kiir na kabila la Nuer linamuunga mkono Machar.

Mkataba wa usitishaji mapigano unaorudiwa mara kwa mara umeshindwa kusitisha mapigano ambayo yameuwa maelfu ya watu na kuwakosesha makazi takribani watu milioni mbili nchini humo.

XS
SM
MD
LG