Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 14:23

Sauti ya Amerika yaadhimisha miaka 70


VOA ilianza kutangaza Februari 1, 1942

Rais wa Marekani Barack Obama aliungana Jumatano na viongozi wengine mashuhuri duniani kuipongeza Sauti ya Amerika katika sherehe za maadhimisho ya miaka 70 tangu shirika hili kubwa la utangazaji duniani lilipozinduliwa.

Rais Obama aliipongeza Sauti ya Amerika kwa kutangaza ukweli wenye msingi katika habari zake hata wakati matangazo yake yanapokabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya serikali za kigeni ambazo zinadhibiti habari kwa raia wao na kuwanyima haki ya kimsingi kama binadamu.

Katika ujumbe kwa njia ya Video rais Obama alisema taifa la Marekani limepata nguvu na dunia kupata msukumo wa kuzingatia haki zaidi kutokana na juhudi za Sauti ya Amerika.

Naye mwanaharakati wa kidemokrasia kutoka Burma Aung San Syu Kyi alisema maadhimisho ya miaka70 ya VOA kwake binafsi na ni kama sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa rafiki yake. Bi. Suu Kyi alisema Sauti ya Amerika na vituo vingine vya utangazaji vilikuwa rafiki wa kutegemewa wakati wa kifungo chake cha nyumbani.

Kiongozi wa kidini kutoka Tibet Dalai Lama, naye aliiambia idhaa ya Tibeti ya Sauti ya Amerika kuwa idhaa hiyo ya Sauti ya Amerika imetekeleza wajibu mkubwa kwa watu wa Tibet kwa kutangaza habari zisizoegemea upande mmoja . Sauti ya Amerika ilianzishwa na serikali ya Marekani wakati wa vita vya pili vya dunia ili kutoa matangazo kwa maeneo yaliyokaliwa na wajerumani wa Nazi.

Tangu nyakati hizo Sauti ya Amerika imeibuka kuwa shirika kubwa la utangazaji wa kimataifa, likitangaza kwa zaidi ya lugha 40 za dunia na kuwafikia wasikilizaji na watazamaji zaidi ya milioni 140 kila wiki.

Matangazo ya kwanza ya Sauti ya Amerika yalipeperushwa hewani katika lugha ya Kijerumani Februari mosi mwaka wa 1942, yakianza kwa maneno yafuatayo… Hii ni sauti kutoka Marekani.. matangazo hayo yaliendelea kuahidi kuwa : Habari hizi huenda zikawa njema. Habari hizi huenda zikawa mbaya. Lakini, tutakueleza ukweli.”

Lakini maadhimisho ya miaka 70 ya Sauti ya Amerika yamefanywa wakati shirika hili la serikali ya Marekani likikabiliwa na kupunguzwa kwa bajeti yake kama ilivyo kwenye idara nyingine za serikali ambapo pia baadhi ya idhaa zinazotangaza kwa lugha mbali mbali zitapunguziwa wafanyikazi wake na idhaa nyingine kufutwa kabisa.

Sauti ya Amerika hutangaza kupitia Radio, televisheni, mtandao wa mawasiliano wa Internet, simu za mkononi na ina washirika wa makampuni ya utangazaji zaidi ya elfu moja na mia mbili kote duniani. Pamoja na wafanyikazi wake 1,100 hapa Washington DC, Sauti ya Amerika ina waandishi habari katika maeneo yenye misukosuko kote duniani .

XS
SM
MD
LG