Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 02:35

Ijue siku ya mtoto wa Afrika


Watoto wakicheza nje ya kambi yao huko Sudan Kusini
Watoto wakicheza nje ya kambi yao huko Sudan Kusini

Tanzania na DRC ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizoadhimisha siku ya mtoto wa Afrika duniani ikiwa na lengo la kumkomboa mtoto kimaisha.

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu , na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanywa kila juni 16 tangu ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya umoja wa Afrika. Elimu kwa watoto ndio imekuwa mada kuu kwa nchi nyingi katika kumuinua mtoto wa Africa.

Mwaka huu nchini Tanzania kumefanyika maandamano ya kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika yaliyoandaliwa na shirika la Planning International kwa kushirikiana na wadau wengine kwa lengo la kuhamasisha Serikali na mashirika binafsi na yale ya kimataifa kusaidia watoto wa mitaani na wale yatima walioachwa na wazazi wao kutokana na sababu mbalimbali kama vile maathiriko ya virusi vya HIV na ukimwi.

Watoto wa mitaani walikusanyika alhamisi na kuandamana katikati ya jiji la Dar es salaam wakisoma risala zao kutoa ujumbe kwa Serikali kusaidia katika kuwapatia elimu na kuwaondolea huduma duni za maisha.

Meneja mawasiliano wa shirika la Planning International, Bwana Tenga Tenga akizungumza na Sauti ya Amerika- VOA, amesema kichwa cha habari katika maadhimisho hayo kilikuwa ni “ tushirikiane kwa pamoja kutatua tatizo la watoto waishio mitaani”. Amesema suala la afya pia limepewa kipaumbele katika maadhimisho ya mwaka huu , ambapo shirika lake kwa kushirikiana na watoto limepaza sauti kuhakikisha kuwa afya bora inatolewa kwa watoto hasa waishio mitaani.

Akizungumzia kuhusu elimu amesema shirika la Planning International limeweza kuwakusanya watoto wa mitaani na kuwasomesha, kuwapatia karo za shule, kuwajengea mabweni ili watoto wengi waweze kupata haki ya kuwa na elimu bora.

Aidha amesema ni zaidi ya miaka kumi sasa tangu maadhimisho haya yaanze na mafanikio yamejitokeza licha ya kwamba kumekuwa na changamoto za hapa na pale. Moja ya mafanikio ni kuwawezesha vijana ambao wamefikia umri wa kujiajiri, linatoa masomo ya ufundi stadi kumfanya kijana kujikomboa kimaisha, linawajengea visima vya maji na hata kuwakusanya pamoja na kuwapatia makazi.

Nako Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo –DRC, hasa eneo la mashariki siku hii ya mtoto wa Afrika imeadhimishwa kwa Serikali ikishirikiana na shirika la umoja wa mataifa la MONUSCO kuwaondoa wasichana watoto waliochini ya umri wa miaka 18 kutumikishwa katika harakati za ngono na vile vile vijana wadogo kutumika kama askari watoto kwenye makundi yatumiayo silaha.

Katika maadhimisho hayo pia Serikali ya DRC imeanza mpango wa kuwatafuta watoto wa mitaani na kuwahesabu ili waweze kuwashughulikia kama kuwapa ajira ndogondogo kama vile useremala na ufundi stadi pamoja na kutoa huduma za elimu.

XS
SM
MD
LG