Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 02:53

Hali ya wasi wasi yapelekea wakimbizi kuingia Rwanda kutoka Burundi.


Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza .
Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza .

Wakati ikiwa imesalia miezi miwili Burundi ifanye uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge, wakimbizi kutoka nchini humo wameanza kukimbilia nchi jirani ya Rwanda, hasa mashariki mwa nchi hiyo. Waziri anayehusika na masuala ya wakimbizi nchini Rwanda Seraphine Mukantabana alithibitisha hayo lakini hakutoa idadi kamili ya wakimbizi wa Burundi waliokwishafika nchini Rwanda.

Unapofika katika kata ya MBYO wilayani Bugesera jimbo la mashariki mwa Rwanda karibu na mpaka wake na Burundi, inakuwa vigumu kutofautisha wakimbizi wanaoikimbia Burundi kutokana na usalama mdogo na wale wanaoingia Rwanda kwa ajili ya kujitafutia shughuli za vibarua kisha kurejea kwao ifikapo jioni.

Hata hivyo wenyeji wanasema kwamba hali hii si ya kawaida kwa sababu idadi ya watu wanaoingia kutoka Burundi inazidi kuongezeka.Wengi wao ni wanawake na watoto.

Mmoja wa wakimbizi hao anasema “Mimi nimekimbia kwa sababu tumekuwa tukielezwa kuwa sisi si watu,isipokuwa vitu vilivyoanguka toka juu, eti tuko kama migomba unayopanda kisha wakati unafika unaikata eti na sisi tutakuwa hivyo hivyo baadae”.

Hali hii imeonekana karibu kwenye mipaka yote baina ya nchi za Rwanda na Burundi hasa upande wa mashariki mwa Rwanda.

Kwa upande wake katibu kata ya MBYO Kalisa Francis amethibitisha kwamba wiki hii waliweza kuzipokeaa familia 8 zenye watu 22 kutoka Burundi kama wakimbizi. Na tayari utaratibu wa kuwapatia mahali pa kukaa unaendelea.

Akizungumza kwa njia ya simu waziri anayehusika na masuala ya wakimbizi nchini Rwanda Bi. Seraphine Mukantabana amethibitisha ujio wa wakimbizi hao lakini hakuweza kufafanua idadi jumla ya watu waliokwishaingia Rwanda mpaka sasa.

Baadhi wanaingia wakisema kwamba wanakimbia,lakini tumegundua kuna hata raia wa Rwanda ambao wamekuwa nchini Burundi kwa muda ambao pia wanaingia kwa kuhofia kile wanachokitaja kama usalama mdogo nchini Burundi.Kwa ujumla warundi wanaingia,hawajaanza kuingia kwa idadi kubwa.

Burundi inafanya uchaguzi mkuu wa mwezi Juni mwaka huu na kama hali itaendelea hivi huenda Rwanda huenda ikapokea wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Burundi.

Wakati huo huo mpasuko mkubwa umetokea ndani ya chama kilichopo madarakani nchini Burundi cha CNDD-FDD baada ya wafuasi wa chama hicho wanaoshikilia nyadhifa mbali mbali serikalini kumtumia barua rais wa sasa wa Burundi Pierre Nkurunzinza wakimtaka aache kugombea muhula mwingine katika uchaguzi wa mwaka huu. Mkuu wa idara ya mawasiliano katika ikulu ya rais amepuuzilia mbali barua hiyo na kusema kuwa hali hiyo ya kumuandikia barua rais ni hali ambayo imezoeleka katika chama chao.

XS
SM
MD
LG