Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 07:00

Ufaransa yashambulia wanamgambo wa Mali


Ndege za kivita za Ufaransa
Ndege za kivita za Ufaransa
Ndege za kivita za Ufaransa zimeshambulia mji mmoja nchini Mali uliotekwa na wanamgambo wa ki-Islam huku majeshi zaidi yakijitayarisha kupigana dhidi ya makundi ya uasi.

Mashahidi wanasema ndege za Ufaransa zilishambulia mji wa Diabaly Jumatatu usiku, saa kadhaa baada ya wapiganaji wa ki-Islam kuchukua udhibiti wa mji huo uliopo kilomita 400 kaskazini mwa mji mkuu wa mali, Bamako.

Maafisa wa ulinzi wa Ufaransa wanasema wanajeshi wa Ufaransa waliopo Mali hivi sasa ni 750 na idadi hiyo huwenda ikaongezeka hadi 2,500. Na Nigeria ilisema Jumanne kuwa itapeleka kundi la kwanza la wanajeshi wake nchini Mali ndani ya muda wa saa 24.

Mataifa ya Afrika Magharibi yanaharakisha mpango wao wa kupeleka wanajeshi nchini Mali baada ya makundi ya ki-Islam ambayo yalidhibiti upande wa kaskazini kuanza kusonga mbele zaidi wiki iliyopita.

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Araud, alisema Jumatatu kuwa Jenerali mmoja wa Nigeria ambaye ataongoza jeshi la Afrika huko tayari yuko mjini Bamako. Nchi jirani za Niger, Burkina Faso na Senegal pia zimeahidi kupeleka majeshi yake nchini Mali.

Ufaransa ilipeleka majeshi nchini Mali siku ya Ijumaa kufuatia ombi kutoka serikali ya muda nchini Mali. Araud anasema serikali iliamua kutoa msaada wa kijeshi kwa sababu ilikuwa na wasi wasi kwamba wanamgambo wangeweza kuteka nchi.
XS
SM
MD
LG