Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 03:05

Wazambia wapiga kura leo


Mkurugenzi wa kamati ya uchaguzi Zambia, Priscilla Isaacs, akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchaguzi mkuu wa Septemba 20, 2011
Mkurugenzi wa kamati ya uchaguzi Zambia, Priscilla Isaacs, akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchaguzi mkuu wa Septemba 20, 2011

Zaidi ya wazambia milioni 5.1 wamejitokeza kupiga kura leo katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani

Wazambia wanapiga kura Jumanne katika kile kinachotarajiwa kuwa uchaguzi wa urais wenye ushindani mkali kati ya Rais wa sasa Rupia Banda na kiongozi wa upinzani Michael Sata.

Rais Banda ana matumaini ya kutumia wimbi la karibuni la mafanikio ya uchumi kumshinda bwana Sata, kiongozi wa kitaifa aliyepewa jina la “King Cobra”, ambaye anaongoza chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Patriotic Front.

Rais Banda anasema sera zake zinahamasisha ukuaji wa uchumi, wakati bwana Sata anamshutumu Rais kwa kuruhusu rushwa na kuwapa mamlaka makubwa zaidi wawekezaji wa kigeni hasa China, mwendeshaji mkubwa wa madini ya shaba nchini Zambia.

Bwana banda na chama chake cha Movement for Multiparty Democracy kilipata ushindi mdogo dhidi ya bwana Sata katika duru ya marudio ya uchaguzi wa mwaka 2008 kuziba nafasi ya marehemu Rais Levy Mwanawasa, ambaye alikufa kutokana na ugonjwa wa kiharusi. Bwana Sata aliyapinga matokeo na wafuasi wake waliandamana kwa siku nne baada ya matokeo.

Bwana Sata karibuni aliwasihi wafuasi wake kulinda kura zao kwa kuendelea kubaki kwenye vituo vya kupiga kura baada ya kupiga kura zao. Anaishutumu tume ya uchaguzi kupanga kuiba kura za urais kwa kutumia karatasi zilizowekwa awali kwenye masanduku ya kura. Tume hiyo imetupilia mbali shutuma hizo.

Gazeti la Times of Zambia linasema maafisa wa uchaguzi wanadai kwamba wale ambao wameshapiga kura zao lazima waondoke mara moja kwenye vituo vya kupigia kura.

Maafisa wa usalama nchini Zambia wamezidisha ulinzi katika vituo vya kupigia kura, wamewapiga marufuku wachuuzi wa mitaani kuuza ulevi na vifaa kama vile mashoka au mashepe ambayo yanaweza kutumika kama silaha. Maafisa wa usalama wanaonya kwamba ghasia zozote zitakabiliwa na nguvu zote za kisheria.

Zaidi ya wa-Zambia milioni 5.1 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani. Mashirika mbali mbali ya kimataifa yapo kufuatilia taratibu za uchaguzi zinavyokwenda.

XS
SM
MD
LG