Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 16:11

Wapinzani 2 wa Sudan Kusini wanashikiliwa na polisi Kenya


Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan Kusini, Taban Deng Gai, kushoto akizungumza na rais Salva Kiir. Julai, 2016.
Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan Kusini, Taban Deng Gai, kushoto akizungumza na rais Salva Kiir. Julai, 2016.

Polisi nchini Kenya wanawazuia wapinzani wawili wa serikali ya Sudan Kusini.

Wakili wao na wanaharakati wa haki za binadamu wamesema Jumatano wote wawili wako hatarini iwapo watarejeshwa nchini kwao.

Mmoja ni wakili wa Sudan Kusini, Dong Samuel, mtetezi wa haki za binadamu na ni mwanachama wa kikundi cha haki za binadamu na amati ya haki ya wapinzani wa Sudan Kusini.

Mwengine ni Aggrey Idri, mwenyekiti wa kamati ya masuala ya haki za binadamu kwa upande wa upinzani.

Samuel mara ya mwisho alionekana Jumatatu jioni, wakati Idri alionekana Jumanne asubuhi.

Wakili wao, Eddy Orinda anaamini kwamba wateja wake wanashikiliwa makao makuu ya polisi Nairobi, lakini amesema hana taarifa zaidi.

“Hakuna mtu amesema iwapo tayari wamefunguliwa mashtaka juu ya kitu chochote. Hakuna anayetoa sababu zozote juu ya uwezekano wa kuwepo amri ya serikali ya kuwaondoa nchini ambayo tumekuwa tukiisikia. Kwa hivyo sote tuko gizani,” alisema Orinda.

Human Rights Watch
Mtafiti wa shirika la kutetea haki za binadamu (Human Rights Watch) Sudan Kusini, Jonathan Pedneault amesema hali ya watu hao inawatia wasiwasi.

“Kwa hiyo tunasababu za msingi kuwa na wasiwasi juu ya kusafirishwa kwao, kwanza kabisa, itakuwa kinyume cha sheria, lakini pia hawa watu wawili wanaweza kupata matatizo watakaporudishwa Sudan Kusini,” amesema Pedneault.

Samuel ni mkimbizi aliyesajiliwa nchini Kenya, kwa hiyo HRW na shirika la Amnesty International wanadadisi suala la kumsafirisha wakisema itakuwa ni uvunjifu wa sheria za kimataifa.

Amnesty imeiambia VOA katika taarifa ya maandishi kuwa “ licha ya hatari ya mateso yatakayowakabili watu hao wakiwa Sudan Kusini, lakini kitendo cha kuwarudisha kitakiuka jukumu la Kenya chini ya makubaliano ya Umoja wa Mataifa dhidi ya utesaji.”

Waziri wa Habari Sudan Kusini

Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei amekanusha kufahamu lolote juu ya kushikiliwa watu hao wawili.

“Sijasikia kitu chochote kuhusu kukamatwa kwao,” alisema Makuei. “Najua wao bado wako Nairobi.”

Juhudi za kuwatafuta wasemaji wa polisi wa Kenya ziligonga ukuta na simu ya waziri wa mambo ya ndani ilikuwa haina majibu.

Iwapo Samuel na Idri watarudishwa, haitokuwa mara ya kwanza kwa Kenya kuwarudisha wapinzani wa Sudan Kusini.

Mnamo Novemba, msemaji wa upinzani James Gatdet alirudishwa Juba, pamoja na kuwa na hadhi ya ukimbizi. Hatima yake ni kwamba amekuwa kizuizini mpaka sasa bila ya kufunguliwa mashtaka yoyote katika makao makuu ya usalama wa taifa.

Pedneault amesema tangu kutokea machafuko huko Juba Julai, kumekuwa na ongezeko la kamatakamata ya wapinzani.

Orinda amesema anaitaka serikali ya Kenya kutoa tamko wakifafanua iwapo ilikuwa na mkono wake katika kutoweka na pengine uwezekano watu hao wawili kurejeshwa Sudan Kusini.

XS
SM
MD
LG