Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 16:06

Huduma za afya kwa wanawake Sierra Leone ni tatizo


Wanawake wajawazito wakiangalia televisheni wakati wakisubiri huduma katika hospitali ya wazazi ya Princess mjini Freetown.
Wanawake wajawazito wakiangalia televisheni wakati wakisubiri huduma katika hospitali ya wazazi ya Princess mjini Freetown.
Wauguzi wanawahudumia wagonjwa katika hospitali hii mjini Makenini, kaskazini mwa Sierra Leone. Serikali ilianza kutoa huduma ya bure ya afya kwa wanawake na watoto kwenye vituo vyote vya afya vinavyoendeshwa na serikali miaka miwili iliyopita. Tangu wakati huo, wanawake kutoka maeneo ya vijijini wamefurika katika vituo vya afya ili kupata fursa ya huduma hizo.
Fedha zinazoendesha program hiyo hadi sasa zinafikia dola milioni 40 nyingi ya fedha hizo zikitolewa na wafadhili kama vile idara ya Umoja wa Mataifa ya kuhudumia watoto UNICEF. Na Umoja wa Mataifa unaelezea kuwa program hiyo imekuwa na mafanikio katika muda mfupi, wakizungumzia kupungua kwa viwango vya vifo vya watoto na wanawake wakati wa kujifungua, idadi hiyo imepungua kwa nusu.
Huduma bure ya afya inatakiwa kulipia gharama zote kwa wanawake wajawazito, kina mama wanaonyonyesha na watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano. Ukijumuisha madawa, huduma kama vile kuhamishiwa hospitali kuu kwa matibabu zaidi, ushauri na kumuona daktari, upasuaji na hata huduma za gari la wagonjwa.
Lakini ripoti ya Amnesty International mwaka 2012 kuhusu Sierra Leone na juhudi za kutoa huduma bure ya afya, inasema wanawake wengi wanaendelea kulipia gharama za dawa, licha ya kuwepo kwa sera ya huduma ya bure.
Adama Koroma ni mmoja wao, anasema muuguzi alimtaka alipie gharama ya dawa kwa mtoto wake kwenye hospitali ya makeni.
“Waliniambia kwmaba hawana dawa hizo, inanilazimu nizinunue mwenyewe. Lakini sikuwa na fedha kwahiyo ilibidi nirudi nyumbani na kuuza baadhi ya vitu vyangu.
Wanawake wa vijijini wanakabiliwa na changamoto zaidi kupata huduma ya afya. Koroma anasema barabara mbaya inafanya iwe vigumu kwa wanawake kutoka vijijini mwao na kwenda kwenye hospitali ya Makeni au kwenye kituo cha afya.
Alipougua Koroma anasema alijaribu kutembea kwa takriban maili sita mpaka kituo cha afya cha karibu. Lakini alijifungulia msituni kwa msaada wa shangazi yake licha ya ukweli kwamba program iliyopo inatoa huduma ya gari kwa wagonjwa.
“ Barabara ilikuwa mbaya sana, sikuweza kuifikia gari ili inifikishe hospitali kwa wakati.”
Fatmata Kanneh ni mkuu wa kitengo cha wazazi katika hospitali ya Makeni anasema kumekuwepo na mafanikio ya wazi tangu program ya huduma ya bure ya afya ianzishwe , na dawa zinapatikana.
“ Siku zote tuna dawa za dharura, hasa kwenye kitengo cha uzazi, hata watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano wanapatiwa tiba. Tuna damu kwenye benki ya damu kwa ajili ya dharura.”
Kuna matatizo tofuati kwa wanawake wa mijini. Katika mji mkuu, Freetown, wagonjwa wanasema huduma za bure za afya haina maana kuwepo kwa huduma za afya.
Katika hospitali ya wazazi ya Princess Christian PCMH, Hawa Lanai anasema yeye na mtoto wake wa kiume Mohammed mwenye umri wa mwaka mmoja wamerudishwa mara nne kutoka hospitali kwasababu hakuna daktari wa kuwaona.
Waziri wa Afya na Huduma ya Usafi wa Sierra Leone, Zainab Hawa Bangura anasema serikali inaangalia masuluhisho kwa baadhi ya matatizo hayo, ambayo yanasababisha ongezeko kubwa katika huduma za afya. anaelezea kwamba kabla ya kuwepo kwa program ya bure , wafanyakazi katika kituo cha PCMH walikuwa wakiwaona wanawake 800 kwa mwaka. Tangu wakati huo, idadi imeongezeka na kufikia wanawake elfu 12.
Amnesty International inazungumzia masuala mengine kama vile ukosefu wa ufuatiliaji, matumizi mabaya ya madawa na kutokuwepo na njia muafaka za kuripoti matatizo katika mfumo.
Bangura anasema serikali pia inafanya kazi kuzungumzia masuala haya. Anasema mfumo mpya haraka utawekwa kwa ajili ya wanawake katika maeneo ya vijijini ambao watakuwa kama wafuatiliaji katika vituo vya afya kwenye jamii zao. Kila mwanamke atapewa simu ya mkononi ambayo itawaunganisha na kituo kikuu cha afya mjini Freetown kuripoti ukiukaji.
XS
SM
MD
LG