Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 11:42

UN: Maeneo yenye njaa Somalia yaongezeka


Familia kutoka maeneo yaliyokumbwa na njaa zikisubiri mpango wa kuelekea kwenye kambi ya wakimbizi kutafuta chakula na malazi huko Mogadishu, Somalia, August 3,2011
Familia kutoka maeneo yaliyokumbwa na njaa zikisubiri mpango wa kuelekea kwenye kambi ya wakimbizi kutafuta chakula na malazi huko Mogadishu, Somalia, August 3,2011

Umoja wa Mataifa unasema maeneo matatu zaidi ya Somalia sasa yanakabiliwa na njaa.Ripoti zinasema kuwa njaa inatarajiwa kuenea zaidi kama hakuna uingiliaji kati wa haraka.

kitengo cha Umoja wa Mataifa cha tathmini ya usalama wa chakula na mradi wa kuonya juu ya njaa ujulikanao kama FEWS-NET unasema njaa huko kusini mwa Somalia inazidi kuwa mbaya.

Takwimu mpya zinaonyesha kwamba watu zaidi wanafariki na kuathiriwa na hali mbaya ya utapiamlo katika mkoa wa Middle Shebele na pia miongoni mwa watu waliopoteza makazi yao huko Mogadishu na eneo la Afgoye magharibi mwa mji mkuu.

Hadi sasa hali ya njaa imetambuliwa katika maeneo mawili tu ya Lower Shebelle na Bakool kusini mwa kati ya Somalia.

Mshauri mkuu wa masuala ya kiufundi katika kitengo cha usalama wa chakula kwa somalia katika Umoja wa Mataifa, Grainne Maloney anasema hali katika jamii za watu waliopoteza makazi yao ni za kusikitisha.

“Ni kundi ambalo kwa kiasi kikubwa tayari limekoseshwa makazi na walikuwa wakitegemea misaada ya kibinadamu, na bila shaka kukiwa na masharti katika kuwafikia na masharti katika ufadhili, hawakuweza kupata msaada. Takriban miaka 3 iliyopita kiwango cha utapiamlo huko kilikuwa takriban asilimia 12 na kuona hivi sasa kiwango hicho kimefikia asilimia 40 inasikitisha.”

Hali ya njaa kimsingi hivi sasa inamaanisha kuwa takriban asilimia 30 ya raia wana utapiamlo, watu majumbani hawana fursa ya kupata chakula na kwamba vifo vimetokea kutokana na njaa.

Hakuna takwimu halisi kuhusu idadi ya vifo vinavyotokea kila siku,lakini inakadiriwa kuwa ni mamia ya watu.

Umoja wa Mataifa imeomba msaada wa zaidi ya dola billion moja kushughulikia mzozo na hadi sasa wamepata takriban asilimia 40 ya fedha hizo zilizoombwa. Maloney anasema msaada zaidi unahitajika haraka.

“Kuna haja ya uingiliaji kati mkubwa hivi sasa kwa vile sasa watu millioni 2.8 huko kusini wanahitaji msaada na hiyo ni pamoja na chakula, lishe bora, maji, afya na vifaa vya kilimo. Wanahitaji kila kitu hivi sasa na hawawezi kusubiri.”

Maloney anasema kuna matumaini kidogo kwa Mogadishu, ambako watu waliopoteza makazi yao wanaweza kufikiwa na mashirika ya misaada ya kibinadam ambayo yanapanua juhudi zao huko.

Mzozo wa Somalia ulisababishwa na mkongo mbaya wa ukame, ambao baadhi wanasema ni mbaya zaidi kuwahi kufanyika katika miaka 60. Lakini ukosefu wa kuwepo serikali inayofanya kazi vilivyo imeifanya hali hiyo kuwa mbaya zaidi na vikwazo vya misaada vilivyowekwa na kundi la Al shabab lenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al Qaida.

Umoja wa Mataifa unategemea njaa kuenea katika maeneo mengine ya kusini mwa Somalia katika majuma manne au sita yajayo na kuendelea hadi mwezi Disemba.

XS
SM
MD
LG