Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 03:47

UN: Wasomali wazidi kuingia Kenya na hali ni tete Djibouti


Umoja wa Mataifa unasema theluthi mbili ya watoto chini ya miaka mitano wanahitaji msaada wa haraka wa chakula
Umoja wa Mataifa unasema theluthi mbili ya watoto chini ya miaka mitano wanahitaji msaada wa haraka wa chakula

Umoja wa Mataifa unasema wakimbizi wa Somalia wanazidi kuingia nchini Kenya licha ya kuongeza juhudi za misaada ya dharura kukabiliana na hali ya ukame na baa la njaa huko kusini mwa Somalia.

Ofisi ya huduma za dharura ya Umoja wa mataifa inasema kwamba katika wiki ya kwanza ya mwezi Agosti, takribani wakimbizi 1,500 wanawasili nchini Kenya kila siku kwenye kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyopo kaskazini mwa Kenya. Hiyo ni idadi kubwa zaidi kuliko ya mwezi wa Julai.

Juhudi za kimataifa za kusaidia baa la njaa zinaonekana kuongezeka haraka katika siku za karibuni, wakati kundi la wanamgambo la al-Shabab limeondoa wapiganaji yake kutoka mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mashirika ya kutoa msaada ya Idara ya chakula Duniani na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR wanasafirsha kwa ndege mahitaji ya dharura hadi Mogadishu na wanapanga safari zaidi za ndege.

Ofisi ya huduma za dharura ya Umoja wa Mataifa ilionya Jumatano kwamba zaidi ya dola bilioni 1.4 bado zinahitajika kukabiliana na ukame katika kanda hiyo, ambao umesababisha watu milioni 12 kuhitaji msaada wa dharura.
Umoja wa Mataifa umetangaza maeneo matano ya kusini mwa Somalia kuwa maeneo yenye baa la njaa na kuonya kwamba baa litaenea zaidi.

Ripoti ya Jumatano pia ilieleza kwamba hali inazidi kuwa mbaya katika nchi jirani ya Somalia, ya Djibouti. Umoja wa Mataifa unasema theluthi mbili ya watoto chini ya miaka mitano walopimwa katika maeneo mawili ya kaskazini wanahitaji msaada wa chakula.

Ripoti ilisema kwamba kwa jumla, Djibouti ni nchi ya pili iliyoathirika na baa la njaa katika eneo la pembe ya Afrika.

XS
SM
MD
LG