Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 22:41

Maafisa waliojizawadia shilingi bilioni 7 Uganda kukiona cha 'mtema kuni'


Eneo la uchimbaji mafuta katika wilaya ya Bulisa, kaskazini magharibi mwa Kampala.
Eneo la uchimbaji mafuta katika wilaya ya Bulisa, kaskazini magharibi mwa Kampala.

Hili ni suala la dharura. Tuliwalipa pesa kama bunge kufanya kazi hiyo. suala hili lazima lichunguzwe na bunge, amesema mbunge Stephen Mukitale.

Bunge la Uganda limeagiza ufanyike uchunguzi wa kina juu ya kadhia inayowakabili watumishi wa serikali waliojizawadia kiasi cha shilingi bilioni 7.

Hii ni baada ya serikali kushinda kesi dhidi ya kampuni ya kuchimba mafuta kutoka Ireland ya Tallow iliyokuwa imekwepa kulipa ushuru wa dola milioni 430.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wetu wa Kampala Kennes Bwire maafisa hao waligawana kisiri kama ni sehemu ya kupongezana.

Madai hayo ya ubadhirifu yanafungamana na sehemu ya pesa ilizolipwa serikali baada ya kushinda kesi dhidi ya kampuni ya kuchimba mafuta ya Tallow katika machimbo ya Albertine, magharibi mwa Uganda.

Kampuni ya Tallow ilikuwa imekwepa kulipa ushuru wa kiasi cha dola milioni 430 na kushtakiwa na serikali katika mahakama mjini London na baada ya mawakili wa serikali kushinda kesi hiyo maafisa hao walijizawadia kiasi cha shilingi bilioni 7.

Malipo haya, yamelikera taifa, ambapo wabunge wamesema kuna maswali mengi ya kujiuliza.

Mbunge Stephen Mukitale amesema: “Hili ni suala la dharura. Tuliwapa pesa kama bunge kufanya kazi hiyo. Swala hili lazima lichunguzwe na bunge.”

Aliongeza kuwa licha ya kwamba waliojizawadia pesa hizo ni watumishi wa umma wanaopokea mshahara kila mwezi kwa kazi wanayofanya, ushahidi uliopo unaonyesha kwamba walimshurutisha rais Yoweri Museveni kuwazawadia.

Mwandishi wa VOA amesema wabunge wanataka kuelezwa sababu zilizopelekea pesa hizo kutolewa kama zawadi licha ya bunge kupitisha bajeti ya shilingi bilioni 10 kama marupurupu, kuwasaidia kufanikisha kesi dhidi ya kampuni ya Tallow.

Amesema wabunge pia wanahoji mbona kila mara watu wengi hupewa zawadi za medali au barua ya kutambua mchangao wao, iweje hawa wanaotajwa wapewe kiasi kikubwa cha pesa.

Kwa mujibu wa taarifa za bunge, wabunge wanasubiri Ijumaa wiki ijayo watakapokutana kwa kikao maalum kuwalazimisha waliopokea pesa hizo kuzirejesha.



XS
SM
MD
LG