Majadiliano kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na upinzani kupitia upatanishi wa viongozi wa Kanisa Katoliki, yaliendelea hadi Ijuma usiku bila ya kupatikana ufumbuzi wa mwisho wa mzozo wa kisiasa nchini humo.
Mzozo huo umezushwa na kukata kwa Rais Joseph Kabila kuondoka madarakani mhula wake ulipomalizika tarehe 19 Disemba 2016, na kukupelekea ghasia kati ya wananchi na vikosi vya usalama katika miji mikuu kwa siku tatu.
Matumaini ya kufikiwa makubaliano yalijitokeza Alhamisi pale upinzani na serikali kukubali kwamba Rais Kabila ataendelea kubaki madarakani hadi kuitishwa uchaguzi hapo disemba 2017.
Viongozi wa pande zote walikubalkiana kwamba Kabila hatoweza kugombania tena uchaguzi na hakuna mabadiliko ya katiba yatafanyika mnamo kipindi cha mpito cha mwaka mmoja.
Kizingiti kikubwa siku ya ijuma kufuatana na mwandishi wa Sauti ya amerika mjini Kinshasa Saleh Mwanamilongo ni kuhusu kuundwa tume ya kufuatilia utekelezaji wa makubaliano. Upinzani wanataka paundwe baraza la kufuatilia mpito kuliko tume na liongozwe na Etienne Tshisekedi, lakini serikali inakubali kuwepo na tume pekee iisiyo na mamlaka makubwa.
Hali ingali tete huko Kongo ambako kuna baadhi ya wananchi waloeleza kuridhika kwao na Kabila kubaki hadi mwakani lakini kutogombania tena uchaguzi,huku wakazi wa mashariki wakisema makubaliano hayo ni ukiukaji wa katiba.