Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 19:52

Obama aikemea vikali Syria na Iran katika UN


Rais Barack Obama akizungumza kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, Sept 25, 2012
Rais Barack Obama akizungumza kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, Sept 25, 2012

Asema Marekani itaendelea kuwasaka wauaji na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na itafanya kila iwezalo kuzuia program ya nyuklia ya Iran

Rais wa Marekani Barack Obama amewataka viongozi wa dunia “kukemea dhidi ya ghasia na ugaidi” akisema dunia inaweza kupata mafanikio kwa kuhamasisha ustahmilivu na uhuru.

Bwana Obama alizungumza jumanne kwenye kikao cha 67 cha mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa. Aliwaambia wajumbe “wakati umefika kuwarekebisha wale ambao pengine hawakuhusika na ghasia na hutumia chuki kwa Marekani au Magharibi”.

Hotuba yake kwa ujumla ililenga katika wiki kadhaa za maandamano ya ghasia yaliyochochewa na filamu moja inayokashifu u-Islam, iliyotengenezwa nchini Marekani. Bwana Obama alisema video hiyo ni mbaya na haipendezi, lakini alisema hiyo haihalalishi ghasia zozote za umwagaji damu ikiwemo kifo cha balozi wa Marekani nchini Libya, Chris Stevens, ambaye aliuwawa katika shambulizi moja kwenye ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi.

Bwana Obama aliapa Marekani “itaendelea bila kusita kuwasaka wauaji na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria”.

Rais huyo wa Marekani pia alitumia maneno makali kwa Rais wa Syria Bashar al-Assad, akiielezea serikali yake kuwa “utawala ambao unawatesa watoto na kufyatua roketi kwenye majengo ya nyumba za makazi”.

Pia aliionya Iran kuwa Marekani “itafanya kila iwezalo” kuizuia Tehran kutengeneza silaha za nyuklia. Alisema “bado kuna muda na nafasi” ya kushauriana juu ya program yake ya nyuklia lakini “muda huo una kikomo”.

Katibu Mkuu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon aliuhutubia mkutano mkuu mapema jumanne akiyataka mataifa wanachama kufanya zaidi katika kupunguza mzozo nchini Syria.

Aliuita mgogoro wa Syria “janga la kieneo lenye madhara kwa ulimwengu” na aliwashutumu wote serikali ya Syria ya Rais Bashar al-Assad na upinzani kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.
XS
SM
MD
LG