Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 13:26

Netanyahu na Putin wakutana uso kwa uso mjini Moscow


Rais wa Russia, Vladmir Putin (R) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wakiwa Kremlin mjini Moscow,
Rais wa Russia, Vladmir Putin (R) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wakiwa Kremlin mjini Moscow,

Rais wa Russia, Vladmir Putin na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu walikubaliana kuratibu hatua za majeshi ya nchi zao ndani na kuzunguka Syria ili kuzuia mapambano yasiyotarajiwa ya kijeshi.

Viongozi hao walikutana Jumatatu kwenye makazi ya Rais wa Russia huko Novo-Ogaryovo, nje ya Moscow. Baadaye bwana Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari kwamba yeye na bwana Putin walikubaliana juu ya njia za kuzuia kutoelewana. Bwana Netanyahu alisema mazungumzo yao yalifanyika katika hali ya kuheshimiana.

Mkutano wa Jumatatu unafuatia ripoti kwamba Moscow imekuwa ikiongeza ndege za kivita na wanajeshi nchini Syria kama sehemu ya juhudi za kuisaidia serikali ya Rais Bashar al-Assad kupambana na majeshi ya waasi yanayojaribu kumuondoa madarakani. Kremlin ilimkariri bwana Netanyahu akielezea wasi wasi juu ya Iran na Syria kulipatia kundi la wanamgambo wa Hezbollah la Lebanon, “silaha za kisasa zinazolenga dhidi ya raia wetu”.

Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu.

Waziri Mkuu huyo wa Israel pia alisema kwamba Iran ikisaidiwa na jeshi la Syria, inajaribu kuunda kile alichokiita “eneo la pili la kigaidi” dhidi ya Israel huko Golan Heights. Bwana Putin alijibu kwamba Syria na jeshi lake wapo katika hali mbaya kiasi kwamba hawana mpango wa “kufungua eneo la pili” dhidi ya Israel, lakini badala yake inalenga “kuuokoa utaifa wake”, Kremlin ilisema.

Pia kiongozi huyo wa Russia alimwambia bwana Netanyahu kwamba anafahamu wasi wasi wake na alifurahi kwamba bwana Netanyahu alikwenda huko ili kuzungumzia masuala haya kwa kina. Kiongozi huyo wa Russia pia alilaani upigaji makombora kwenye eneo la Israel.

XS
SM
MD
LG