Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 11:06

Waziri Ummy Apendekeza Dawa ya Ndoa za Utotoni


Waziri Ummy Mwalimu
Waziri Ummy Mwalimu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema bila ya kuwapeleka wazazi mahakamani na kuhukumiwa kifungo, ndoa za utotoni haziwezi kukomeshwa.

Waziri amesistiza kwamba iko haja ya kuchukua hatua stahiki kwa wahusika wanaochangia ongezeko la ndoa za utotoni hapa nchini, akisema marekebisho ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni lazima yafanyike.

“Ni muhimu sheria hii irekebishwe ili kuweza kuhakikisha mtoto wa kike anapata stahiki yake kubwa ambayo ni elimu.”

Ametaka wahusika wampelekee taarifa za nchi nzima kuhusu walimu wakuu wangapi wamewasilisha taarifa zao kama sheria inavyowataka kuhusu watoto walio olewa kabla ya kumaliza shule.

“Na sheria hii imeenda mbali kwani mwalimu mkuu yoyote ambaye hajatoa taarifa ametenda kosa la jinai na yeye amewekewa adhabu,” amesema.

“Ingekuwa sheria iko chini ya wizara yangu tayari ningekuwa nimeipeleka ikafanyiwe marekebisho bungeni,” aliongeza.

Lakini amesema kwamba ataendelea kuwasiliana na wizara ya katiba na sheria katika hatua za kuifanyia mabadiliko sheria hii ndogo.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa kumefanyika uzinduzi wa utafiti wa ndoa za utotoni uliofanywa na mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali na Umoja wa Mataifa.

Ameeleza kuwa utafiti huo umefanywa ili kubaini changamoto zinazochangia kuwepo tatizo hilo la ndoa za utotoni kwa watoto wa kike nchini Tanzania, linalonyima mtoto wa kike kupata elimu na kuwa huru kuchagua mustakabli wa maisha yake.

Kwa mujibu wa mtafiti Dkt Lucas Kagera wa shirika lisilo la kiserikali la utafiti REPOA, ambalo ni mdau mkubwa katika utafiti wa ndoa za utotoni, inakidirwa watoto 36 kati ya mia moja huolewa kabla ya kufikisha miaka kumi na nane na wengine 27 kati ya mia hupata mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, huku mikoa ya shinyanga na Mara ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya ndoa za utotoni.

Mikoa ambayo inatatizo kubwa la ndoa za utotoni iliohusishwa na tafiti ni pamoja na Shinyanga, Tabora, Mara, Dodoma na Lindi. Na mikoa mingine miwili ilikuwa kati ya ile ambayo tatizo hili la ndoa za utotoni ni dogo.

Mtafiti huyo amesema lengo ilikuwa kuona ni kwa nini tatizo ni kubwa katika hiyo mikoa mitano na sababu zinazopelekea hilo tatizo kuwepo, na pia ile mikoa inayo onekana kufanya vizuri kidogo tuone ni nini tunaweza kujifunza.

Changamoto ya mila na desturi pia ni moja ya sababu za kuwepo ndoa za utotoni kwa watoto wa kike hapa nchini kama anavyoeleza binti Specioza Maganya aliyeshiriki katika uzinduzi wa ripoti hiyo.

Kwa ujumla wadau na washirika wa maendeleo wanaoshughulika na masuala ya haki za mtoto wa kike wametakiwa kuhakikisha wanafanya kazi vijijini ambako kuna waathirika wakubwa wa ndoa na mimba za utotoni.

Imeandaliwa na Mwandishi wetu DINA CHAHALI, Tanzania

XS
SM
MD
LG