Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 09:52

Mlipuko wa bomu waua 60 Libya


Wapiganaji wa waasi wakionekana ndani ya mji wa Tripoli nchini Libya
Wapiganaji wa waasi wakionekana ndani ya mji wa Tripoli nchini Libya

Lori lililokua na milipuko na kuendeshwa na mjitoa mhanga limeuwa watu wasiopungua 60 kwenye chuo kimoja karibu na mji wa Misrata uliopo kaskazini-magharibi mwa Libya. Hakuna mtu yeyote anayedai kuhusika na tukio hilo. Shambulizi hilo limetokea wakati kundi la ugaidi la Islamic State likiendeleza mashambulizi yake kwenye viwanda vya mafuta katika eneo la mashariki.

Ripoti inaeleza kwamba kiasi cha watu 400 wengi wakiwa polisi vijana wanaopatiwa mafunzo walikusanyika Alhamis kwenye chuo hicho cha mafunzo katika mji wa Zliten, wakati mlipuaji wa kujitoa mhanga alipolipua bomu hilo.

Wakazi wa mji huo walisaidia kuwasafirisha waathirika kwenda hospitali zilizo karibu katika mji wa Misrata. Ni shambulizi lililosababisha vifo vingi tangu kuondolewa madarakani kwa Moammar Ghadhafi mwaka 2011.

Mashambulizi ya aina hiyo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika miezi ya karibuni ambapo wanamgambo wa ki-Islam wanatumia nafasi ya kukosekana utawala kuendesha shughuli zao.

Video iliyochapishwa kwenye mtandao Alhamis inaonekana ikionesha wanamgambo wanaotii kundi la Islamic State wakiteka mji wa Pwani wa Bin Jawad ambao ni muhimu kijeshi. Lakini mchambuzi Riccardo Fabiani kutoka Eurasia Group alisema kupanuka kwa kundi huko Libya ni katika eneo dogo tu. “Tatizo kwa kundi la IS nchini Libya ni kwamba hakiwezi kufaidika na mgawanyiko wa kidini kama ilivyo huko Irak na Syria. Na muhimu zaidi, kiwango cha uungaji mkono ambao wanapata kutopka kwa wananchi wa Libya ni kidogo sana”.

Moshi umetanda angani katika maeneo ya mashambulizi nchini Libya
Moshi umetanda angani katika maeneo ya mashambulizi nchini Libya

Katika siku za karibuni wanamgambo wa Islamic State wamefanya mashambulizi kwenye viwanda vikubwa vya mafuta huko Es Sider na Ras Lanuf na kusababisha moto mkubwa. Maafisa katika miji hiyo wanasema kila lori linabeba mapipa 460,000ya mafuta.

“Mkakati wao hapa ni kushambulia voiwanda hivyo na kuviharibu. Kwa nini wanafanya hivyo hivi sasa, ni wazi kabisa, kwa sababu kuna mkataba wa Amani, kuna serikali ya umoja wa kitaifa na huu ni wakati wa kuharibu na kuhujumu mafanikio yaliyopatikana hadi sasa”.

Utawala unaopingana nchini Libya, mmoja wenye makao yake mjini Tripoli unaungwa mkono na makundi ya ki-Islam na mwingine ni serikali inayotambulika kimataifa iliyopo mjini Tobruk, zimetia saini mkataba unaosimamiwa na umoja wa mataifa wa kushirikiana madaraka mwezi uliopita, lakini bado hawajaunda serikali ya umoja.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa Libya, Martin Kobler, alitoa wito kwa wa-Libya kuunga mkono mkataba wa kushirikiana madaraka na kuungana dhidi ya ugaidi.

XS
SM
MD
LG