Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 13:55

Mkurugenzi mtendaji bodi ya mikopo ya wanafunzi Tanzania afutwa kazi


Waziri wa elimu Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako
Waziri wa elimu Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako

Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya elimu sayansi, teknolojia na ufundi imesema imebaini udhaifu mkubwa wa kiutendaji katika bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini Tanzania unaosababisha migomo ya mara kwa mara ya wanafunzi wa vyuo vikuu.

please wait

No media source currently available

0:00 0:02:33 0:00
Kiungo cha moja kwa moja


Kufuatia udhaifu huo uliobainika katika bodi ya mikopo , Waziri wa elimu, sayansi, teknolojia na ufundi Profesa Joyce Ndalichako, amesitisha mkataba wa ajira wa mkurugenzi mtendaji wa bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, George Nyatega.

Aidha Profesa Ndalichako amewasimamisha kazi wakurugenzi wengine watatu ambao ni mkurugenzi wa fedha na utawala Yusuph Kisare, mkurugenzi wa urejeshaji mikopo Juma Chagonja pamoja na mkurugenzi wa upangaji na utoaji mikopo Onesmo Laizer.

Akitoa uamuzi wa wizara hiyo Profesa Ndalichako alisema taarifa ya mkaguzi wa ndani mkuu wa serikali ya mwaka 2013 ilibaini mapungufu makubwa katika usimamizi wa fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi.

Baadhi ya udhaifu uliobainika ni wanafunzi 23 walipata mikopo kupitia vyuo viwili tofauti kipindi cha miaka mitatu mfululizo huku bodi pia ikitoa mikopo kwa wanafunzi 343 wasiokuwa na usajili kwenye vyuo husika.

Profesa Ndalichako alisema udhaifu mwingine uliobainika ni pamoja na wanafunzi 19,348 walipata mikopo bila kupitishwa na kamati ya mikopo na wanafunzi 54,299 walipangiwa mikopo wakati hawakuwa wameomba.

Wizara ya elimu, sayansi, teknolojia na ufundi pia imetoa angalizo kwa vyuo vikuu vyote vya umma na binafsi nchini Tanzania ambavyo vingine kuna taarifa za wao kushirikiana na bodi ya mikopo kuhujumu fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Wizara sasa itateua maafisa watakaoshika nafasi hizo kwa muda hadi uchunguzi utakapokamilika na wakurugenzi hao wa bodi ya mikopo kuchukuliwa hatua stahiki.

XS
SM
MD
LG