Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 12:49

Milipuko ya mabomu yavuruga mbio za Boston Marathon



Milipuko miwili ya mabomu iliyotokea karibu na mstari wa kumaliza mashindano ya mbio za Boston Marathon, nchini Marekani imewauwa watu wawili na zaidi ya 50 wengine walijeruhiwa Jumatatu.

Maafisa wa usalama walisema mlipuko wa tatu ulitokea kwenye maktaba ya John F.Kennedy iliopo katika mtaa mwingine wa Boston. Hakuna majeruhi yeyote aliyeripotiwa kutokana na mlipuko wa tatu na bado haijafahamika vyema kama mlipuko huo unahusiana na milipuko miwili iliyotokea awali kwenye mji huo.

Polisi wa Boston hawakusema kama milipuko ilikuwa sehemu ya shambulizi la ugaidi. Msemaji wa polisi alisema timu ya wataalamu wa kutegua mabomu walikuwa wakichunguza mifuko na vifurushi vilivyoachwa kiholela kwenye tukio la milipuko ya awali lakini hakuna vifaa vingine vyovyote vinavyohusiana na milipuko vilivyopatikana.

Picha za televisheni zilionesha matukio ya kuogopesha, mtaa ulijaa vifusi na damu, wafanyakazi wa huduma za dharura wakiwa wamebeba machela waliwasili mara moja kwenye mahala uharibifu mkubwa ulipotokea.

Milipuko ilitokea mmoja baada ya mwingine ikipishana sekunde chache tu karibu na eneo la kumaliza mashindano ya mbio ambayo yaliwashirikisha wanamichezo wapatao 27,000. Mashindano yalisitishwa baada ya milipuko kutokea pamoja na usafiri wa njia ya metro katika eneo hilo.

Rais Barack Obama amelihutubia taifa na kutoa rambi rambi zake kwa waathiriwa akiahidi kwamba wahusika wa tukio hilo watapatikana, watafikishwa mbele ya sheria na watafahamu kwa nini wamefanya kitendo hicho kiovu.

Wakati huo huo polisi nchini Ungereza wanasema wanatathmini mipango ya usalama kwa ajili ya mbio za marathon zitakazofanyika Jumapili mjini London, baada ya milipuko ya mabomu kutokea huko Boston na kusababisha vifo vya watu wasiopungua wawili.

Waandaaji wa marathon mjini London wanasema wamewasiliana na polisi kuzungumzia mipango ya usalama mara tu waliposikia tukio la milipuko la Boston nchini Marekani.

Maelfu ya wanariadha wamepangiwa kushindana katika mbio za London Marathon, zitakazofanyika chini ya muda wa wiki moja.
XS
SM
MD
LG