Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 23, 2024 Local time: 09:56

Mgogoro wazuka bungeni Tanzania


Wabunge wa bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania bila kujali itikadi ya vyama vyao, Jumatatu wamegomea kuendelea na kikao na kutoka nje ya bunge, mara baada ya naibu spika wa bunge Dk. Tulia Akson kuzima hoja ya kufukuzwa chuoni kwa wanafunzi wa diploma wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Wakiongea na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa bunge mara baada ya bunge kusitisha kikao chake, wabunge Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki, Esther Bulaya wa Bunda na Stanslaus Mabula wa Nyamagana, wamepinga hatua ya Naibu Spika kutotaka kuwasikiliza wabunge, ambao ndio wawakilishi wa wananchi.

Mapema Jumatatu mara baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni, mbunge wa Arumeru Mashariki Bw. Nassari aliomba muongozo wa spika kuhusu bunge lijadili jambo la dharura kuhusiana na kufukuzwa chuoni kwa wanafunzi wa hao, Naibu Spika akakataa na ndipo wabunge wa upinzani wakasimama kupinga.

Kutokana na hali hiyo, ndipo Naibu Spika akaagiza askari wamemtoe nje mbunge huyo wa Arumeru Mashariki, jambo ambalo halikuungwa mkono na wabunge wengi walioamua kutoka nje na kusababisha lisitishe kikao chake.

Akitoa ufafanuzi wa sakata hilo la wanafunzi hao, waziri wa elimu Profesa Joyce Ndalichako amesema, walimu ndio waliogoma kuwafundisha wanafunzi na kudai serekali imefanya jitihada kutatua mgogoro huo japo hazikufanikiwa kwa sababu ya waalimu kuidai serekali madai yanayoelezwa hayakuwa sahihi kwa mujibu wa mkaguzi wa hesabu za ndani.

Amesema serekali haiwezi kumuingilia mkaguzi wa ndani hasa ikizingatiwa waalimu wameonyesha kutokuwa tayari kuwafundisha wanafunzi hao na wanafunzi tayari wameshakaa bila kusoma kwa hiyo serekali imeona ni busara kwa wanafunzi kurudi makwao wakati ufumbuzi wa tatizo hilo ukiendelea kupatikana.

XS
SM
MD
LG