Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 10:20

Mchora vibonzo mashuhuri ‘Juha Kalulu’ afariki dunia nchini Kenya


Mfano wa vibonzo vya 'Juha Kalulu'
Mfano wa vibonzo vya 'Juha Kalulu'

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la nchini Kenya, Bwana Gitau ambaye anafahamika na wengi kwa jina la Kisanii la Juha Kalulu alifariki dunia siku ya Jumanne saa kumi jioni katika hospitali ya wilaya ya Gatundu ambako alikuwa amelazwa baada ya kuugua.

Gitau ndiye mwanzilishi wa vibonzo maarufu vya Juha Kalulu ambavyo vimekuwa vikichapishwa kwenye magazeti nchini Kenya kwa miongo kadhaa.

Gazeti la Taifa Leo, limekuwa likichapisha katuni zange tangu lilipoanzishwa hadi wakati wa kifo chake.

Kazi ya msanii huyo ilianza kuchapishwa kwenye gazeti la ‘Baraza’ kabla ya kuhamia kwa ‘East African Standard’ na hatimaye kwa gazeti la Nation mwaka wa 1961. Baada ya gazeti la Kiswahili la Taifa Leo, kuzinduliwa, Gitau alihamia kule.

Gitau alizaliwa katika kijiji cha Gichuka katika ya Kiambu mnamo Desemba 8, 1930 na kujiunga na shule ya msingi ya Kamwangi, Kiambu, kisha Kabaa School wilayani Machakos kwa darasa la nne.

Aliendelea na masomo yake ambapo baadaye alielekea Githunguri kijiunga na Taasisi ya Ualimu 1947.

Mmojawapo wa walimu wake ni aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya, Mzee Jomo Kenyatta.

Gitau amenukuliwa akisema kuwa alianza uchoraji katuni kitaaluma mnamo 1954.

Asili ya Juha ‘Kalulu’

Juha ni jina la Kiswahili linalotumika kuashiria ujanja na kwa kiasi upumbavu fulani na Kalulu ni jina la sungura katika lugha ya Kinyasa, inayotumika nchini Malawi. Gitau aliyatumia maneno hayo kutoa ujumbe na hata ushauri wa kila aina kupitia michoro yake.

Gazeti la Nation limeripoti kwamba Marehemu Gitau alijifunza lugha ya Kinyasa alipokuwa akifanya kazi nchini Tanzania karibu na mpaka wa Malawi, katika miaka ya hamsini (1950s).

Kando ya katuni zake kuchapishwa magazetini, marehemu mzee Gitau aliweza pia kuchapisha vitabu.

Msanii Gitau ameacha watoto kumi na mmoja.

XS
SM
MD
LG