Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 19:56

Mapigano yanaendela mashariki mwa DRC


Waasi wa M23 wakiwa nje ya nyumba katika kijiji cha Kanyaruchinya, kilomita 6 kutoka Goma, November 18, 2012.
Waasi wa M23 wakiwa nje ya nyumba katika kijiji cha Kanyaruchinya, kilomita 6 kutoka Goma, November 18, 2012.
Mapigano mengine yamezuka karibu na mji wa Goma huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC, baada ya serikali ya DRC kupuuza madai ya mazungumzo ya amani kutoka kundi la waasi wa M23.

Mwandishi wa habari wa Sauti ya Amerika-VOA anasema kulikuwa na ufyatuaji risasi mkali Jumatatu kiasi cha kilomita tatu kutoka mji wa Goma na karibu na uwanja wa ndege. Msemaji wa kundi la M23,Vianney Kazarama aliiambia VOA kwamba kundi la waasi linadhibiti sehemu ya kaskazini-mashariki mwa Goma.

Pia kuna ripoti za ufyatuaji risasi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda. DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwasaidia waasi wa M23 huku Rwanda ikiendelea kukanusha shutuma hizo.

Wapiganaji wa M23 wamesonga mbele kilomita chache kuingia Goma katika muda wa siku chache zilizopita baada ya kuyarudisha nyuma majeshi ya serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo, Idara ya Watoto ya Umoja wa Mataifa-UNICEF inasema vita vikali vinavyoendelea huko Goma mashariki mwa DRC vimelazimisha maelfu ya watu ambao tayari wamepoteza makazi yao kukimbia kwa mara nyingine.

UNICEF inasema ina wasiwasi juu ya athari za kisaikolojia ambazo watoto wa Congo watakabiliwa nazo. Nona Zicherman mkuu wa UNICEF anayeshughulikia masuala ya dharura huko Kinshasa anasema wasiwasi wao mkuu ni hali ya wanawake na watoto ndani na karibu ya Goma, ambao wameathirika na mapigano na pia wasiwasi juu ya usalama wa wafanyakazi wao.

Anasema maelfu ya watu tayari wamekimbia maeneo ya watu waliopoteza makazi yao kilomita kadhaa kutoka Goma.Zichermann anasema UNICEF inajua kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya raia waliokwenda Goma kutafuta hifadhi na kwamba walikuwa wakiwasaidia katika kambi ya Kanyaruchinya iliyopo nje ya Goma ambayo ni makazi ya takriban watu elfu 60.

Anasema japo hawana idadi kamili wanajua kuwa idadi kubwa ya raia wa Kanyaruchinya na vijiji jirani pia wamekimbilia Goma na wamefika katika sehemu kadhaa na wanaishi na familia zilizowapa hifadhi katika mitaa ya Goma.

UNICEF tayari inatoa misaada kwa mamia ya wanawake na watoto wanaotafuta hifadhi katika kituo cha Don Bosco Catholic Center huko Goma. Zicherman anasema UNICEF tayari ina mipango ya dharura kwa sababu katika siku za nyuma ugonjwa wa kipindupindu umewahi kuwa tatizo hapo huko Goma na pia kwenye kambi ya Kanyaruchinya.
XS
SM
MD
LG