Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 07:35

Mahakama ya Kenya yakataa kuzuia uteuzi wa Jaji Mkuu


Bunge la Kenya litakaloidhinisha uteuzi wa wakuu wa mahakama Alhamisi
Bunge la Kenya litakaloidhinisha uteuzi wa wakuu wa mahakama Alhamisi

Mahakama kuu ya Kenya imekataa kutoa amri ya kusitishwa uteuzi wa Jaji Mkuu na naibu wake ulotangazwa Jumanne, kutokana na mashtaka yaliyofikishwa na wakili Harrison Kinyanjui.

Mahakama kuu iliamrisha kuidhinishwa haraka utreuzi huo kutokana na dharura iliyopo nchini Kenya katika masuala ya mahakama.

Bw Kinyanjui aliwasilisha mashtaka kwa msingi kwamba tume ya idara ya sheria inayosimamia kazi za uteuzi wa maafisa wa vyeo vya juu katika wizara ya sheria ilikiuka mamlaka yake na kuchukua hatua kinyume cha sheria.

Mwandishi wa Sauti ya Amerika mjini Nairobi Mwai Gikonyo anaripoti kwamba katika muda wa majuma kadhaa yaliyopita tume maalumu ya kuajiri wafanyakazi wa idara ya mahakama imekuwa ikiwahoji watu waliowasilisha maombi ya kuteuliwa kwenye nyadhifa za Jaji Mkuu, naibu wake pamoja na kiongozi wa mashtaka.

Tume imependekeza majina ya mawakili wawili mashuhuri nchini humo, ili kuchukua nyadhifa hizo. Watu hao ni wanasheria na wakereketwa wa haki za binadamu ambao ni Dr.Willi Mtunga na Bibi. Nancy Baraza, ambao wakati wa utawala wa mzee Daniel Arap Moi, waliwekwa kizuizini kwa kuipinga serikali ya chama cha KANU.

Rais Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga, wameunga mkono uteuzi huo. Pia baadhi ya wanasiasa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamekubaliana na majina ya watu walioteuliwa kuchukua nyadhifa hizo.

Lakini baadhi ya wanasiasa ikiwa ni pamoja na muungano wa madhehebu mbali mbali ya kidini wanapinga uteuzi wa Dr.Wili Mtunga kama Jaji Mkuu, wakidai kuwa Dr. Mtunga hakustahili kuteuliwa kuchukua nyadhifa hiyo kwa sababu ya tabia na maadili yake yasiyofaa.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba Dr.Mtunga ambaye zamani alikuwa mhadhiri wa sheria katika chuo kikuu cha Nairobi, anatabia ya kuvaa vipuri kwenye maskio yake.

Waziri wa zamani wa kilimo nchini Kenya, William Ruto anasema wananchi wa Kenya wanastahili kujihadhari na Jaji Mkuu mwenye kuvaa vipuri maskioni. Ruto anadai uteuzi huo unakiuka maadili ya kijamii na katiba ya taifa. “ikifika kiwango anayechaguliwa kusimamia mahakama ya Kenya ni mwanamme mwenye amevaa vipuri katika maskio yake, anaezungumza na majini kupitia vipuri hivyo, basi mjue tunahitaji dua kama taifa.”

Vile vile Baraza kuu la Makanisa nchini Kenya linapendekeza kwamba Rais Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga, wanastahili kuwachunguza kwa makini watu walioteuliwa kuchukua nyadhifa za jaji mkuu na naibu wake, kwa sababu baraza hilo lina mashaka juu ya tabia na maadili ya watu hao.

XS
SM
MD
LG