Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 06:56

Maandamano yazusha ghasia Burundi


Maandamano yaliyozusha ghasia kati ya polisi na wananchi wanaompinga Rais Nkurunzinza asiwanie tena uongozi
Maandamano yaliyozusha ghasia kati ya polisi na wananchi wanaompinga Rais Nkurunzinza asiwanie tena uongozi

Polisi nchini Burundi walitumia mabomu ya machozi na mabomba ya maji Ijumaa kutawanya mamia ya waandamanaji wanaopinga uwezekano wa Rais Pierre Nkurunzinza kuwania awamu ya tatu ya urais, kinyume na katiba ya nchi hiyo ambayo imeweka kiwango cha awamu mbili tu.

Mamia ya watu walijitokeza kuandamana katika mitaa ya mji mkuu Bujumbura Ijumaa kuitikia wito wa makundi ya kiraia na vyama vya kisiasa kujitokeza katika hatua ya kumwekea Rais Nkurunzinza shinikizo asigombanie awamu ya tatu. Rais Nkurunzinza aliingia madarakani mwaka 2005 baada ya miaka 12 ya mapigano nchini Burundi.

Rais Nkurunzinza hajatamka rasmi kama atagombania tena uongozi katika uchaguzi mkuu mwezi Juni lakini wachambuzi wanaamini kuwa kiongozi huyo atatangaza ugombea wake wiki chache kabla ya uchaguzi.

Polisi katika mitaa ya Burundi
Polisi katika mitaa ya Burundi

Polisi walitanda mitaani Ijumaa kukabiliana na mamia ya waandamanaji na baada ya muda walianza kufyatua mabomu ya machozi na mabomba ya maji kutimua waandamanaji. Waandamanaji walilazimika kuingia katika maduka kuepuka moshi wa mabomu ya machozi lakini baadaye wakarudi tena mitaani.

Watu wengine waliwatupia mawe polisi lakini polisi hatimaye walifanikiwa kutawanya maandamano hayo.

Mvutano katika swala hilo umesababisha Warundi zaidi ya 8,000 kukimbilia nchi jirani za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutafuta hifadhi kwa madai kuwa wanahofia usalama wao nchini Burundi kabla ya uchaguzi.

XS
SM
MD
LG