Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 08:31

Kenya yamkamata msafirishaji madawa ya kulevya


Kutoka kushoto: Baktash Akasha, Gulam Hussein, Ibrahim Akasha and Vijaygiri Goswami
Kutoka kushoto: Baktash Akasha, Gulam Hussein, Ibrahim Akasha and Vijaygiri Goswami

Polisi nchini Kenya inamshikilia mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya, Mohamed Jibril aliyekuwa safarini kuelekea Dubai.

Mshukiwa huyo amekamatwa Alhamisi usiku katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi mjini Mombasa akisafirisha dawa za kulevya aina ya “Heroine” alizokuwa amezificha katika viatu.

Kwa mujibu wa kikosi cha polisi cha kuzuia madawa ya kulevya thamani ya madawa hayo yanakadiriwa kuwa dola 100,000.

Rais Kenyatta aonya

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahi ya VOA ameripoti kuwa hivi karibuni Rais Uhuru Kenyatta akiwa Mombasa alikemea vikali ulanguzi wa dawa za kulevya ambao umekithiri katika eneo la pwani ya Kenya.

“Na mtaona mengine na yale ambayo tumeanza, watu wajue ya kwamba watatafuta nchi nyingine, sio Kenya kufanya biashara hiyo,” alisisitiza Kenyatta.

Mwandishi wetu ameongeza kusema kuwa Marekani imekuwa ikiwakosoa watu mashuhuri nchini Kenya kuhusiana na biashara za dawa za kulevya, ikiwa pia kuna taarifa kwamba husafirishwa kwa meli.

Familia ya Akasha

Wakati hatua hizo zikichukuliwa tayari wiki hii familia ya Akasha ambayo watoto wao wawili na washirika wao wawili raia wa nje wanaoshukiwa kufanya biashara hiyo haramu tayari wamekabidhiwa kwa serikali ya Marekani.

Baktash Akasha, Ibrahim Akasha, pamoja na raia wa Pakistan, Ghulam Hussein na Vijaygiri Goswami wa India walikamatwa wiki iliyopita.

Watu hao wanne wanatakiwa kujibu mashtaka katika mahakama moja ya New York, kwa kuhusishwa na ulanguzi wa biashara haramu ya madawa.

Mama wa watoto hao

Mama wa familia ya Akasha anadai tuhuma hizo za ulanguzi wa kimataifa wa dawa za kulevya, ni fitina na uzushi mtupu na anaitaka serikali ya Kenya iingilie kati akitaka watoto wake warudishwe nyumbani.

“Si kweli wanavyotangazwa ni watu wabaya, watu wanatoa maneno ya uongo uongo, na pia kuleta fitina,” amesema mama huyo Fatma Akasha.

Ameongeza kuwa: “Sidhani kama rais wetu na naibu wake wanafurahia hilo la kusafirishwa watoto wetu, hawa pia wanaelewa vizuri na walituhakikishia sisi nchi yetu inajitawala. Naomba basi serikali inisaidie.”

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Josephat Kioko, Kenya.

XS
SM
MD
LG