Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 15:34

Kenya: Vitisho vya al-Shabab vinasababisha bunge kuimarisha usalama


Wapiganaji wa Al-Shabab wakionesha silaha zao wakiwa wanafanya mazowezi yao kaskazini ya Mogadishu
Wapiganaji wa Al-Shabab wakionesha silaha zao wakiwa wanafanya mazowezi yao kaskazini ya Mogadishu

Wakuu wa bunge la Kenya waliamua kuimarisha usalama katika majengo ya bunge kufuatia malalamiko kwamba hakuna ukaguzi wa kutosha wa kuingia katika majengo na usalama umelega lega.

Uwamuzi huo ulichukuliwa baada ya mkutano ulofanyika Ijuma katika afisi ya spika wa bunge na kuhudhuriwa na maafisa wakuu wa polisi, waziri wa usalama wa ndani George Saitoti pamoja na viongozi wa bunge.

Mkutano huo umefanyika siku moja baada ya wabunge kuwasilisha malalamiko mbele ya kamati inayohusika na kazi za bunge juu ya usalama wao wakiwa ndani ya majengo matatu ya bunge.

Tukio hilo linatokea pia wakati serikali ya Kenya ilitangaza kwamba inatafakari juu ya uhusiano wake na Eritrea, kufuatia tuhuma kwamba nchi hiyo inawapelekea silaha wapiganaji wa Al-Shabab huko Somalia.

Waziri wa mambo ya nchi za nje Moses Wetangula alimuita balozi wa Eritrea nchini Kenya Beyene Russom, kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma hizo. Balozi Russom amekanusha tuhuma hizo akisema hazina msingi wowote.

Akizungumza na Sauti ya Amerika Bw Wetangula anasema serikali ya Kenya itawasilisha habari za ukiukwaji huo kwa Jumuia ya Ushirikiano na Maendeleo wa Kikanda, IGADD pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kenya amesema "Kenya inapendelea kuwa na uhusiano mzuri na majirani zake, ndio maana Eritrea ina ubalozi wake Nairobi, lakini mienendo ya serikali ya Eritrea kidogo haijaturidhisha, hasa kwanza msimamo wao wa kutokubali kuitambua serikali ya mpito ya Somalia."

XS
SM
MD
LG