Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 13:35

Wanaojihusisha na ukahaba Kenya waandamana kudai haki zao


Wanaharakati wanaofanya biashara ya ukahaba nchini Kenya wakiandamana mjini Nairobi kudai haki zao. Machi 6,2012
Wanaharakati wanaofanya biashara ya ukahaba nchini Kenya wakiandamana mjini Nairobi kudai haki zao. Machi 6,2012

Kundi moja la makahaba nchini Kenya limeandamana kudai haki za watu wanaojihusisha na biashara ya ukahaba nchini humo

Wakenya wanaofanya biashara ya ukahaba waliandamana kwenye mji mkuu Nairobi, Jumanne wakidai kupewa heshima kwa kazi yao wanayoifanya na kutendewa vyema na serikali.

Wanaharakati katika kundi hilo wanasema ni suala la haki ya binadamu, lakini baadhi ya watu waliokuwa wakishuhudia maandamano hayo hawakushawishika na suala hilo.

Kundi la wanawake na wanaume wasiopungua 40, wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa vitambaa vya rangi nyeusi na machungwa walizuia usafiri wa magari wakati wa saa za asubuhi zenye harakati nyingi na kuwapa watu hamasa ya kutaka kujua zaidi juu ya biashara ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu katika mji mkuu wa Kenya lakini nadra kutajwa.

Maandamano hayo yalifuatia maandamano kama hayo yaliyofanyika katika siku kadhaa zilizopita katika mataifa mengine, ikiwemo Afrika Kusini na Namibia kama sehemu ya vuguvugu la kimataifa la wafanyakazi wa ukahaba.

Mfanyakazi mmoja wa kiume katika kundi hilo alisema “leo ni siku ya haki za wafanyakazi wa ukahaba. Tunataka biashara hii isichukuliwe tena kuwa ni uhalifu kwa sababu ya bugudha za polisi, unyanyapaa, nafasi ya kupata huduma za afya, huduma za sheria”.

Dottie mwenye umri wa miaka 28, mfanyakazi wa zamani wa ukahaba hivi sasa ni mwanaharakati wa taasisi ya haki za jamii iitwayo Fahamu. Anasema maandamano haya ni kuhusu haki za msingi za binadamu.

“Nchini Kenya na sehemu nyingine barani Afrika, hasa Afrika mashariki, wafanyakazi wa huduma za ukahaba hawatambuliwi kama binadamu. Wanabaguliwa sana. Wanabughudhiwa na hawana hata uwezo wa kupata huduma za sheria katika matukio ambayo wamekuwa wakibughudhiwa, wamekuwa wakibakwa.”


Ukahaba ni kinyume cha sheria nchini Kenya, lakini wafanyakazi wa huduma za ukahaba wapo kila mahali kwenye mitaa ya mji mkuu na kwenye baa na hoteli zenye hadhi ya juu.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Meya wa jiji la Nairobi George Aladwa alipendekeza kuhalalisha ukahaba baada ya kupokea orodha ya malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa ukahaba katika jiji hilo. Muda si mrefu alibadilisha msimamo wake, kufuatia upinzani mkali wa wananchi na alisema polisi wataendelea kuwasaka wale wanaotajwa kuwa ni “ wasichana wanaojiuza” na wateja wao.

XS
SM
MD
LG