Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 18:37

Rais wa Mexico Akutana na Wajumbe Wawili wa Rais Trump


Kutoka kushoto, Waziri wa Usalama wa Ndani John Kelly na Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson
Kutoka kushoto, Waziri wa Usalama wa Ndani John Kelly na Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson na Waziri wa Usalama wa Ndani, John Kelly wamekutana Alhamisi na Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto na wajumbe wa baraza lake la mawaziri.

Hatua hii ni kile kinachotegemewa kuwa ni mwanzo wa mikutano mingi ya ngazi za juu, kuzungumzia masuala ya dawa za kulevya, biashara na uhamiaji kati ya nchi hizi mbili.

Mawaziri wawili muhimu katika baraza la Rais Donald Trump wanategemea kuondoa wasiwasi na kupunguza ghadhabu zilizoenea kutokana na sera mpya za uongozi wa Marekani zilizoelekezwa Mexico.

“Ni muhimu kuwa rais anawapeleka mawaziri wake Mexico mapema wakati huu wa uongozi wake,” Msemaji wa White House Sean Spicer amesema Jumatano. “Ni alama ya mahusiano yenye tija kati ya mataifa yetu mawili.”

Spicer pia ameelezea mahusiano kati ya nchi hizi mbili kuwa “ni imara na yenye nguvu.”

Kuharibika Mahusiano

Safari hii imekuja kwa kile kinachoonekana kama ni kuharibika kwa mahusiano kati ya nchi hizi mbili, ambazo zilikuwa na masikilizano mazuri na zikishirikiana mpaka wenye urefu wa kilomita 3,100 tangu vita kati ya nchi hizo mbili katika miaka 1840.

Trump amerejea kusisitiza kuwa Mexico, kwa namna moja au nyengine, lazima walipe gharama za kujenga ukuta, jambo ambalo wabunge Washington wanakadiria itagharimu sio chini ya dola za Kimarekani bilioni 12.

Na ni wiki hii tu, Wizara ya Usalama wa Ndani iliainisha sera ambazo zingepelekea kuwaondoa mamilioni ya wahamiaji wasiokuwa na vibali vya kuishi nchini.

Mexico Hawatosita Kupeleka Malalamiko

Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico Luis Videgaray amesema nchi yake haitokubali pendekezo jipya kuhusu wahamiaji lililotengenezwa na Marekani “peke yake” na hawatosita kupeleka suala hilo Umoja wa Mataifa.

“Hili ni jambo lililo haribu sana mahusiano ya Marekani na Mexico, na ni hatua ya ghafla ya kuzorotesha mahusiano yaliyodumu kwa zaidi ya miaka 30,” amesema Shannon O’Neil, Mtafiti wa ngazi ya juu katika tafiti za Amerika ya Kusini kwenye Baraza la Mahusiano ya Nje.

Waziri Kelly

Waziri Kelly ambaye ni jenerali mstaafu wa Majeshi ya Majini, alikuwa na maelewano mzuri ya muda mrefu na viongozi wa Mexico kutokana na kazi yake ya awali kama mkuu wa majeshi ya Marekani katika Kikosi cha Kusini.

Kabla ya kuelekea Mexico, alikwenda Guatemala kukutana na Rais Jimmy Morales na kushuhudia kuwasili kwa waliorejeshwa na wizara ya Usalama wa Ndani kwa ndege ya serikali mji wa Guatemala.

Waziri Tillerson
Maafisa wa serikali ya Marekani wamesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Tillerson, ambaye alikuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la mafuta na gesi, na Kelly watazungumzia suala la usalama katika mipaka, ushirikiano wa vyombo vya usalama na biashara pamoja na mambo mengine.

Mbali na kukutana na Rais Nieto, mawaziri wa Marekani pia wamepangiwa kukutana na mawaziri wa Mexico, idara za mahusiano ya nje, hazina, ulinzi wa taifa na jeshi la majini.

XS
SM
MD
LG