Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 13:44

ICC kutangaza hatma ya washukiwa wa Kenya Jumatatu


Jengo la mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC huko The Haque
Jengo la mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC huko The Haque

Mahakama ya ICC itatangaza iwapo kuna ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi ya uhalifu dhidi ya washukiwa hao

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC inasema itaamua Jumatatu ikiwa washukiwa sita wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya watashtakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu huko The Hague.

Mahakama hiyo yenye makao yake The Hague imesema Ijumaa kwamba itafanya mkutano kutangaza iwapo kuna ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka washukiwa wote au baadhi yao.

Washukiwa hao sita ambao ni pamoja na maafisa wa serikali waliopo madarakani hivi sasa na wa zamani, pamoja na wafanyabiashara wanashutumiwa kwa kupanga ghasia kufuatia uchaguzi wa mwaka 2007 uliokuwa na utata.

Katika ghasia hizo zaidi ya watu 300,000 walikoseshwa makazi na watu 1,300 wengine waliuwawa. Ghasia zilizuka baada ya wakosoaji kudai Rais aliyeko madarakani Mwai Kibaki aliiba kura na hivyo kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo dhidi ya Waziri Mkuu Raila Odinga. Viongozi hao wawili baadaye walikubaliana kuunda serikali ya umoja ya kushirikiana madaraka nchini Kenya.

Uamuzi wa mahakama utakuwa na athari kubwa katika uwanja wa kisiasa nchini Kenya. Washukiwa watatu ni washirika kutoka chama cha Rais Kibaki cha Party of National Unity-PNU. Wengine watatu wengine waliunga mkono chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement-ODM, cha Waziri Mkuu Raila Odinga.

Wakati huo huo washukiwa wawili kati ya sita, Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta na waziri wa zamani wa kilimo, William Ruto wanapanga kuwania nafasi ya kiti cha Rais katika uchaguzi mkuu ujao.

Waziri Mkuu Raila Odinga pia ametangaza atawania kiti cha rais katika uchaguzi ujao, ambao bado haijajulikana utafanyika mwishoni mwa mwaka huu au Machi mwaka 2013.

Baadhi ya wananchi wanakhofu kwamba ghasia huwenda zikazuka ikiwa upande wowote utahisi uamuzi wa mahakama sio sahihi au umeshindwa kuwachukulia hatua za kisheria wale waliohusika na ghasia hizo.

XS
SM
MD
LG