Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 16:00

Lema apata dhamana baada ya miezi minne kizuizini


Godbless Lema
Godbless Lema

Hatimaye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amepata dhamana baada ya kukaa mahabusu kwa miezi minne.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Ijumaa, imetoa dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Kesi hiyo iliyovuta mamia ya watu mahakamani ilihudhuriwa na mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe na katibu mkuu wake, Dk Vincent Mashinji, mawaziri wakuu wastaafu Frederick Sumaye na Edward Lowassa, wabunge na wajumbe wa kamati kuu wa chama.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kulikuwa na ulinzi mkali nje ya eneo la mahakama.

Habari hizo zimeeleza kuwa wananchi wengi wamelalamika kuwa wamezuiliwa kuingia mahakamani kwenda kusilikiza kesi ya Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Jonathan Lema.

Vyanzo hivyo pia vimesema ziko taarifa za baadhi ya waandishi kuwekwa chini ya ulinzi na wananchi wengine kukamatwa.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa katika hukumu yake, Jaji Salma Maghimbi, alisema anatoa dhamana kwa Lema kwa sababu dhamana ni haki yake.

Mahakama Kuu Arusha, ilitoa dhamana kwa Lema akitupilia mbali rufaa iliyoombwa na mawakili wa serikali kupinga Lema kupata dhamana.

Akimpa dhamana, Jaji Maghimbi alitoa masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alitakiwa kuweka bondi ya sh milioni moja pamoja na Lema mwenyewe.

Baada ya hukumu hiyo, mawakili wa serikali waliwasilisha ombi la kufuta rufaa yao iliyowasilishwa mahakamani hapo Desemba 23, mwaka jana kupinga mahakama hiyo kutoa rufaa.

Wakati huo huo mwenyekiti wa chadema taifa Freeman Mbowe amewalaani askari polisi kwa kuwapiga wananchi waliokuja kusikiliza kesi hiyo na kuahidi kuwa suala hilo atalifikisha bungeni.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Khaleed Abubakar Famau, Tanzania

XS
SM
MD
LG