Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 09:26

Chama cha CUF chamtimua mbunge Hamad Rashid


Mbunge wa Wawi Zanzibar Hamad Rashid Mohamed (katikati),akiwa na wanachama wenzake katika kikao cha Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF)mjini Zanzibar
Mbunge wa Wawi Zanzibar Hamad Rashid Mohamed (katikati),akiwa na wanachama wenzake katika kikao cha Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF)mjini Zanzibar

Kiongozi wa CUF, anasema amesikitishwa na vitendo vya Hamad, huku mbunge huyo waWawi akidai hakupewa nafasi ya kujitetea.

Aliyekuwa mbunge wa Wawi visiwani Zanzibar nchini Tanzania, Bwana Hamad Rashid Mohamed amesema uamuzi uliochukuliwa na baraza kuu la chama cha upinzania cha CUF kumfukuza uanachama yeye na wanachama wengine wanne ni kinyume cha katiba ya chama.

Amesema baraza limetoa uamuzi huo bila kuzingatia amri ya mahakama kwa sababu wakili wake alikuwa amefungua ombi mahakamani kusimamisha taratibu zote za kikao cha baraza la chama mpaka pale maandalizi rasmi yatakapokuwa yamekamilika upande wake na kuamuru kuwa kikao kingeweza kuendelea tena baadae mwezi huu.

Chama hicho kimejikuta kimetumbukia katika mvutano na malumbano ndani ya chama huku Bwana Rashid akituhumiwa kuwa mchochezi mkubwa wa kusababisha mgogoro ndani ya chama.

Mbunge waWawi anasema "kila mtu anaetuhumiwa lazima apewe haki ya kujitetea. Sasa mimi sikupewa haki ya kujitetea. Manake niliomba nipewe muda, niliomba niweze kuleta mashahidi, niliomba nilete documents ya kuthibitisha madai yangu, sikupata haki hiyo."

Lipumba asikitishwa na uwamuzi wa Hamad

Ibrahim Lipumba
Ibrahim Lipumba

Kiongozi wa chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa katika ziara ya kikazi mjini Washington anasema amesikitishwa sana na hatua za Hamad, kutoikana na kwamba kabla ya kuondoka Tanzania alikutana na mbunge huyo pamoja na viongozi wa chama na kujadili mvutano uliyopo na alimueleza kwamba haridhiki na taratibu anazofuata.

Lipumba ameiambia Sauti ya Amerika kwamba alipoondoka alikuwa na uhakika kwamba wamelitanzua tatizo hilo na aliamini tatizo halitakuwepo, na kwamba wameshaelewana.

Lakini anasema baada ya kuondoka "pakawa na maelezo zaidi, na maelezo yanayotolewa kwenye vyombo vya habari na mimi aliniandikia barua ambayo kwa kweli sikuielewa kwamba yeye anataka kugombania nafasi ya Katibu Mkuu."

Kiongozi wa CUF anasema jambo hilo halina tatizo lakini uchaguzi wa viongozi wa chama utafanyika mwaka 2014, hivyo inabidi anasema viongozi kuheshimu na kufuata nidhamu na katiba ya chama.

Anasema "ili kujenga demokrasia ni lazima tuwe na vyama vyenye nidhamu, viongozi wenye nidhamu, viongozi wanaofuata katiba, viongozi wanaofuata taratibu." Na hivyo anasema ingawa hayuko Tanzania lakini anaunga mkono uwamuzi ulochukuliwa na baraza kuu la chama.

XS
SM
MD
LG