Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 11:03

Bunge jipya Somalia laanza kazi


Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed(C) akipeana mkono na mwakilishi maalumu wa UN kwa Somalia, Augustine Mahiga(R)
Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed(C) akipeana mkono na mwakilishi maalumu wa UN kwa Somalia, Augustine Mahiga(R)

Serikali kuu ya muda iliundwa mwaka 2004 na haijaweza kuwa na nguvu ya kutosha kuleta uthabiti nchini humo

Bunge jipya la Somalia limeanza kazi jumatatu wakati nchi hiyo inasonga mbele na mpango wa kuunda serikali thabiti ya kudumu.

Kamati ya uchaguzi imewataja wabunge 225 kati ya viti 275 vilivyopo lakini maafisa wanasema idadi hiyo inatosha kwa bunge kufanya kikao chake.

Katika mahojiano na Sauti ya Amerika-VOA waziri wa katiba na maridhiano, Abirahman Hosh Jibril anasema wabunge wapya watamchagua spika na manaibu ifikapo Agosti 27 na Rais mpya wa Somalia ifikapo mwanzoni mwa mwezi Septemba.

Nchi hiyo imevuka tarehe ya mwisho ambayo ni jumatatu ya kumchagua spika mpya na Rais chini ya mpango uliopendekezwa na Umoja wa Mataifa ili kumaliza mamlaka ya serikali ya muda iliyohudumu kwa miaka minane.

Hata hivyo, maafisa wa Umoja wa Mataifa na washirika wa kimataifa walitoa taarifa ya matumaini jumapili wakisema Somalia ina fursa ya kipekee ya kuleta amani na uthabiti.

Mwezi uliopita wajumbe 825 wa bunge walipitisha katiba mpya.

Somalia imekuwa katika miaka 20 ya vurugu na mgogoro tangu wababe wa kivita walipompindua Rais Mohamed Siad bare mwaka 1991.

Serikali kuu ya muda iliundwa mwaka 2004 na haijaweza kuwa nguvu ya kutosha na kuleta uthabiti katika nchi iliyoharibiwa na vurugu kwasababu ya mapigano sugu ya ndani.

Usalama umeimarika katika mji mkuu, Mogadishu tangu jeshi la Umoja wa Afrika lilipolisukuma nje kundi la wanamgambo la al-Shabab mwaka jana. Lakini kundi hilo bado linafanya mashambulizi ya mara kwa mara mjini humo.
XS
SM
MD
LG