Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 14:06

Muhammad Ali afariki akiwa na miaka 74


 Muhammad Ali akipambana na Joe Frazier, Manila, Philippines, Oct. 1, 1974.
Muhammad Ali akipambana na Joe Frazier, Manila, Philippines, Oct. 1, 1974.

Muhammad Ali, bingwa wa ndondi wa zamani katika uzito wa juu, amefariki dunia Ijumaa usiku akiwa na umri wa miaka 74. Ali alishika ubingwa wa dunia mara tatu katika maisha yake.

Kifo chake kilithibitishwa na msemaji wa familia Bob Gunnell baada ya bingwa huyo kulazwa hospitali mapema wiki hii kutokana na matatizo ya kupumua.

Ali, alikuwa bondia mwenye machachari ambaye aliburudisha wapenzi wa ndondi duniani kwa uhodari wake, maneno makali na ya mzaha dhidi ya wapinzani wake, na uchezaji wa ndondi akichanganya spidi na uwezo wa kusema atamwangusha mpinzani wake katika raundi gani.

Oct. 30, 1974: Muhammad Ali akimwangusha George Foreman katika pambano lao Kinshasa, Zaire.
Oct. 30, 1974: Muhammad Ali akimwangusha George Foreman katika pambano lao Kinshasa, Zaire.

Tangu miaka ya kati ya 1960 Ali alikuwa mmoja wa mtu anayejulikana kuliko wote duniani, na ingawa katika miaka ya karibuni alipunguza kusafiri kuonekana kwake ilikuwa jambo lililofurahisha wengi kote duniani.

Kifo chake kimekuja baada ya kupambana muda mrefu na ugonjwa wa Parkinson, unaosababisha kutetemeka. Ali aligundulika kuwa na ugonjwa huo mwaka 1984, miaka mitatu baada ya kuacha ndondi. Alianza ndondi akiwa mtoto wa miaka 12 katika mji wa Louisville, Kentucky, baada ya kuibiwa baiskeli yake.

Ameacha watoto tisa, ikiwa ni pamoja na binti yake Laila, ambaye kama baba yake alikuwa bingwa wa dunia katika ndondi kwa wanawake, na mke wake wa nne, Lonnie.

Katika miaka ya mwisho ya 1960 Ali ambaye alikuwa akijulikana kama Cassius Clay alibadili dini kuwa mwislamu na kuchukua jina la Muhammadi Ali, aligoma kuingia katika jeshi la Marekani kwenda vitani Vietnam, alishiriki kwa vitendo kupigania haki za raia Marekani.

Alichukua ubingwa wa dunia kwa mara ya kwanza mwaka 1964 baada ya kumpiga Sonny Liston na kuushtua ulimwengu akiwa kijana wa miaka 22 tu.

Mapambano yake katika miaka ya baadaye na bingwa mwingine maarufu Joe Frazier, ambaye pia ameshafariki, yamebaki hadi leo kuwa mapambano ya ndondi za uzito wa juu yanayokumbukwa sana.

Mwaka 1974 alimshinda George Foreman katika pambano lililofanyika Kinshasa, Zaire (wakati ule) katika pamobano ambalo linakumbukwa kuwa moja ya mapambano makali sana katika historia ya ndondi.

XS
SM
MD
LG