Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 12:56

Mubarak apatiwa matibabu Ujerumani


Vyombo vya habari vya Misri vinasema Rais Hosni Mubarak amefanyiwa upasuwaji na kutolewa kibofu nyongo bila ya matatizo. Ripoti zinasema kiongozi huyo wa muda mrefu wa Misri alifanyiwa matibabu hayo katika hospitali ya chuo kikuu cha Heidelberg Ujerumani siku ya Jumamosi baada ya kumkabidhi madaraka waziri mkuu wake. Shirika la habari la Reuters linanukulu pia msemaji wa hospitali akisema upasuaji umefanyika vizuri.

Rais Mubarak alieleza kuumwa hapo Ijumaa alipokua kwenye ziara rasmi ya Ujerumani na baada ya kupimwa iliamuliwa inabidi afanyiwe upasuaji. Vyombo vya habari vya Misri vimeeleza kuwa Waziri Mkuu Ahmed Nazif atashikilia uongozi wa taifa hadi kurudi kwa bw Mubarak. Alikua Ujerumani kwa mkutano na Chancela Angela Merkel siku ya Alhamisi.

Rais Mubarak amekua madarakani tangu 1981 na hajamtaja atakae chukua nafasi yake na hivyo kuzusha uvumi juu ya nani huwenda akachukua uongozi wa nchi baada ya muhula wake kumalizika mwakani.

Habari za kupasuliwa kwa rais Mubarak zimesababisha uungaji mkono mkubwa kwa kiongozi huyo huko Misri. Shirika la habari la Associated Press limemnukuu spika wa bunge Fathi Serour akisema mamilioni ya wa-Misri wanamuombea Bw Mubarak uzima na kurudi nyumbani kwa salama.

Hii si mara ya kwanza kumekuwepo na wasi wasi juu ya hali ya afya ya Bw Mubarak, lakini serekali imekua ikijaribu sana kuzuia habari au uvumi wowote kuenea.
Mhariri wa gazeti huru la Misri la Al-Dustour, Ibrahimi Elissa alihukumiwa kifungo cha jela 2008 kwa kuchapisha makala yanayoeleza kwamba rais wa Misri hayuko katika hali nzuri ya afya. Baadae rais alitoa msamaha kwa Elissa.

Muhula wa rais Mubarak unamalizika mwakani na watalamu wengi wa kisiasa wanaamini amekuwa akimtayarisha kijana wake Gamal kuchukua madaraka. Lakini inaonekana Gamal hana umashuhuri miongoni mwa wamisri, na Bw Mubarak alisema mapema wiki hii kwamba mkuu wa zamani wa idara ya nishati ya nuklia ya Umoja wa Matiafa Mohamed ElBaradei ana uhuru wa kupigania kiti cha rais, almradi tu afuate masharti ya uchaguzi wa nchi hiyo.

XS
SM
MD
LG