Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 09:41

Olara Otunnu arejea Uganda.


Mwanasiasa mkongwe Olara Otunnu alirejea Uganda Agosti 22, baada ya kuishi nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 23.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uganda, Matias Kaseija aliwaambia waandishi wa habari mjini Kampala kuwa Bw. Olara Otunnu hatapewa makaribisho makubwa kama watu wengine wanavyotarajia.

Hii imefuatia kauli za wanasiasa nchini humo hasa wale kutoka chama cha UPC ambacho kiliwahi kuongozwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Dr. Milton Obote.

Bwana Otunnu aliwahi kuukana uraia wa Uganda mara alipotofautiana na serikali kuu inayoongozwa na Rais Yoweri Museveni. Bwana Otunnu aliwahi kuiwakilisha Uganda kwenye Umoja Mataifa katika nyadhifa mbali mbali, lakini hatimaye akaanzisha shirika binafsi la kuwanusuru watoto duniani katika maeneo yaliyokumbwa na mizozo.

Chama cha UPC kilitangaza nia ya kumshawishi mwanasiasa huyo kugombea kiti cha urais mwaka 2011, endapo atakubaliwa kugombea nafasi hiyo kuu ya serikali, itabidi achunguzwe na idara za sheria ikiwa hana hatia yeyote. Bwana Otunnu alizaliwa mwaka 1950 katika wilaya ya Kitgum kaskazini mwa Uganda.

Mapema mwezi Julai mwaka huu alikwenda Uingereza na Marekani kuwashawishi raia wa Uganda wanaoishi huko ili kuimarisha msimamo wa kampeni yake ya kutaka kuwania urais.

Viongozi kadhaa wa vyama vya siasa nchini Uganda wamekuwa kimya kuhusu kurejea kwa Bwana Otunnu.

Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti wa chama tawala cha NRM, Kapteni George Michael Mukula ameelezea kuwa chama chake hakina wasiwasi na kurejea kwa Bwana Otunnu nchini Uganda.

Kapteni Mukula aliiambia Sauti ya Amerika kwamba ni vyema ieleweke kwamba Bwana Otunnu ameishi nje kwa muda mrefu kwahiyo angesubiri kwa muda kabla ya kujiingiza katika siasa za nchi kwa vile kuna mabadiliko makubwa katika siasa za Uganda.

XS
SM
MD
LG