Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 22:09

Watu kadhaa wafariki kutokana na mgomo wa madaktari Kenya


Madaktari wakizungumza na polisi wakati wa mgomo
Madaktari wakizungumza na polisi wakati wa mgomo

Kati ya watu 14 hadi 20 inaripotiwa tayari wamepoteza maisha kutokana na mgomo wa madaktari na wafanyakazi wa afya Kenya ambao unaingia nusu wiki sasa tangu uanze.

Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta alivunja ukimya wake Jumatano katika mgogoro huo na kuwataka madaktari kurudi kazini kuyapa nafasi mazungumzo baina ya chama cha madaktari na serikali.

Akizungumza katika uzinduzi wa Chuo Cha Madaktari Mjini Makindu, mashariki ya Kenya, Rais Kenyatta alisisitiza: “Ni lazima tuwe na huruma na maisha ya wananchi wenzetu, ni kwa nini tumekubali zaidi ya watu 14, au karibia 20 kupoteza maisha.

Rais Uhuru Kenyattta
Rais Uhuru Kenyattta

“Kwa wafanyakazi wa umma, hasa madaktari na wauguzi waliogoma hakuna kiongozi wa serikali aliyekataa kuzungumza nao. Nyote mmeshuhudia katika masiku machache yaliyopita, tumekuwa tukifanya kila tunaloweza kumaliza mgogoro huu,” alisema Rais Kenyatta.

Mahakama ya Kazi yaamuru viongozi wa mgomo kukamatwa

Lakini duru za habari nchini Kenya zimeripoti kuwa Mahakama ya Kazi nchini Kenya imeamuru viongozi wote katika huu mgomo wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Kutokana na shinikizo hilo katibu wa Muungano wa Wahudumu wa Afya, Wanafamasia na Madaktari wa Meno, KMPPDU, Dr Ouma Oluga amenukuliwa akisema wao hawatashiriki katika mazungumzo yoyote.

Kauli ya Rais Kenyatta imekuja huku kukiwa na ripoti za kuongezeka kwa hali mbaya katika mahospitali mengi nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kusimamishwa huduma za dharura. Pia kumekuwa na madai kwamba mahakama imeshinikizwa kutoa agizo hilo kutokana na agizo la Rais leo.

Waandishi wa VOA walioko Kenya wameripoti kuhusu wagonjwa kukosa matibabu katika hospitali za Mombasa, Kisumu na Nairobi pamoja na huduma za matibabu kusitishwa katika hospitali za umma kote nchini kufuatia mgomo huo.

Mgonjwa katika hospitali Mombasa
please wait

No media source currently available

0:00 0:00:35 0:00
Kiungo cha moja kwa moja

Mwanzoni mwa wiki hii, madaktari wa Kenya waliungana chini ya Muungano wa Wahudumu wa Afya, Wanafamasia na Madaktari wa Meno, KMPPDU na kugoma kutoa huduma mpaka pale serikali itakapo heshimu mkataba wa makubaliano ya pamoja CBA (Collective Bargaining Agreement); makubaliano yaliyotiwa saini kati ya serikali na madaktari miaka mitatu iliyopita.

Wanaoshiriki katika mgomo wapata 5000

Madaktari, wauguzi, wafamasia, madaktari wa meno na wataalamu wengine wa afya ambao idadi yao inafika 5000 wamesitisha huduma hizo za afya na kuathiri zaidi ya vituo vya huduma za afya 2700 nchini Kenya ambapo wagonjwa wamelazimika kwenda kutafuta huduma hiyo katika hospitali za binafsi.

Kwa mujibu wa Mwandishi wa VOA madaktari hao walikuwa wamebeba bango linalosema daktari sio punda wakielekea katika barabara kuu za Nairobi ili kushinikiza serikali kuu kutekeleza mkataba wa makubaliano uliofikiwa mwaka 2013.

Dr Ouma Olunga ambae ni mmoja wa Madaktari ambaye amejiunga na mgomo alisema:“Sisi kama madaktari,tunataka haya makubaliano yatimizwe na madaktari walipwe malimbikizo yao ya miaka mitatu.”

Askari wa kuzuia fujo wawasambaratisha waandamanaji

Lakini Mwandishi wa VOA alioko Nairobi anasema jaribio la kuendelea kuandama lilitibuka kwani askari wa kutuliza fujo waliwatupia mabomu ya kutoa machozi na kuwasambaratisha. Juhudi zao za kuandamana hadi Wizara ya Afya zilifikia ukingoni.

Hata hivyo maadamano haya yanatokana na kufeli kwa mkutano ulioahidi kutafuta suluhu hivi karibuni, kwani maafisa wakuu wa vyama vya madaktari waligoma kuhudhuria.

Madaktari katika mgomo
Madaktari katika mgomo

Dr Zephania Ashira, Mtumishi wa afya aliyegoma alikaririwa akisema: “Tumekuja kupigania haki za wakenya katika nchi hii, kwa sababu mara nyingi madaktari wanafanya kazi nyingi katika hali ngumu sana na ili hali hawalipwi ipasavyo.”

Aliongeza kusema kuwa: “ Kwa hivyo tunahimiza serikali itoe pesa ili madaktari waungane na serikali kutoa huduma kwa wananchi.”

Hata hivyo madai ya Madaktari ni kuhusu kufanya kazi katika mazingira hatarishi na pia kutokulipwa kwa mujibu wa taaluma zao.

Walipofariki saba patajwa

Miongoni mwa wagonjwa waliofariki saba inadaiwa vifo vyao vilitokana na kukosekana huduma baada ya shughuli kusimama katika hospitali muhimu nchini Kenya. Hata hivyo wako wagonjwa ambao walilazimika kutafuta matibabu hospitali nyingine baada ya kutohudumiwa mara baada ya mgomo kuanza.

Miongoni mwa waliofariki, wanne walikuwa wakitibiwa katika hospitali za Kiambu na Mbagathi. Mgonjwa mmoja alithibitishwa kufariki mjini Kisumu huku wengine wawili wakiripotiwa kufariki dunia eneo la Kinango, katika kaunti ya Kisumu.

Vyombo vya habari vya Kimataifa vinaripoti kwamba katika sakata hilo baadhi ya wauguzi wanataka walipwe kati ya shilingi mia tatu na mia nne ili kuwaosha vidonda wagonjwa waliofika katika hospitali ya umma eneo hilo huku waliolazwa katika hospitali za umma eneo la Rift Valley wakishauriwa kuondoka hospitalini humo.

Waziri wa Afya Cleopa Mailu amenukuliwa na vyombo vya habari vya Kenya akisema hata hivyo anasisitiza kuwa mgomo huo si halali kwani unakiuka agizo la mahakama na kuongezea kuwa kwa sasa serikali inashirikiana na mashirika mbalimbali ya afya kuwanusuru wagonjwa hadi pale suluhu itakapopatikana

XS
SM
MD
LG