Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 11:09

Edward Lowassa ateuliwa rasmi mgombea urais CHADEMA


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemuidhinisha rasmi Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa, kuwa mgombea wa umoja wa vyama vinavyounda UKAWA, na kumteua mwanasiasa wa siku nyingi kutoka chama cha wananchi CUF, Juma Hajji Duni kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Hata hivyo, Bwana Duni alilazimika kujiengua kutoka chama chake cha CUF na kujiunga na CHADEMA ili kutimiza masharti ya kisheria ambayo yanataka wagombea kuwa wanachama wa chama kimoja cha siasa.

Tukio hilo limekuwa la kihistoria kufanyika toka kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mwaka 1992. Wagombea hao wamepitishwa kwa kishindo na kuungwa mkono na vyama vyote vinavyounda umoja wa UKAWA.

Bwana Lowassa na Duni wameahidi kuipeperusha vyema bendera ya UKAWA katika kile walichosema ni muda wa kuhakikisha chama tawala kinaondoka madarakani.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA, Bwana Freeman Mbowe, amesema safari ya kuwapata wagombea hao haikuwa rahisi, bali ilitawaliwa na milima na mabonde. Alisema pia dhamira yao ni kuwatimizia Watanzania ndoto ya muda mrefu.

Aliposimama kushukuru uteuzi wake, Bwana Lowassa amesema sasa anajiona mtu mwenye furaha na hamasa kubwa kwa kukaribishwa kwa kishindo katika ulimwengu mwingine wa siasa na pia ana matumaini makubwa ya kutwaa dola la Tanzania.

Naye mgombea mwenza Bwana Duni amewaambia watanzania kwamba muda sasa umefika wa kukaribisha mageuzi nchini humo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na vyama rafiki kutoka barani Afrika na Ulaya, wanadiplomasia wa nchi za magharibi, viongozi wa kidini na viongozi wote wa UKAWA akiwemo Makamu wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

XS
SM
MD
LG