Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 09:42

Kagame asema usaliti una matokeo yake.


Rais wa Rwanda alipokuwa akipiga kura.
Rais wa Rwanda alipokuwa akipiga kura.
Rais Paul Kagame wa Rwanda ameonya wale wote wanaokula njama za kuhatarisha serikali yake na taifa kwa ujumla yatawageuka wenyewe kabla ya kufikia azma yao. Kauli ya Rais Paul Kagame imekuja huku kukiendelea shutuma kutoka kwa wapinzani kwamba serikali yake ikawa ilihusika na mauaji ya mkuu wa zamani wa ujasusi nchini Rwanda Kanali Patrick Karegeya aliyeuwawa nchini Afrika Kusini. Serikali ya Rwanda ilikanusha madai hayo.

Rais Kagame alitoa kauli hiyo mjini Kigali kwenye kongamano la viongozi wa serikali na madhehebu mbalimbali katika maombi ya kuliombea taifa na kumshukuru Mungu kwa mwaka uliopita. Rais Kagame ambaye alikuwa mzungumzaji wa mwisho kwenye kongamano hilo la siku moja amesema kamwe hatakuwa salama mtu yeyote atakayethubutu kuisaliti Rwanda kwa lengo la kuangamiza maisha ya wanyarwanda wasio na hatia kwa maslahi binafsi.

Amesema nchi hiyo imetoka kwenye dimbwi la mauaji na mateso ya kila aina na kujijenga kufikia hatua ilikofikia leo, huku akiongeza yeyote mwenye dhamira ya kubomoa mafanikio hayo yatamgeuka mwenyewe kabla ya kufikia azma yake.

Alisema “Huwezi kulisaliti taifa na ukadhani utakaa salama,yeyote atakayejaribu atakabiliwa na nguvu tulizopewa na Mungu kuilinda nchi yetu.Yeyote atakayejaribu atakiona hata wale ambao bado wako hai wasubiri - ni suala tu la muda”.

Bila kutaja majina Rais Kagame amesema viongozi wa Rwanda wamekuwa wakitumia muda wao kukanusha shutuma dhidi ya Rwanda kuhusu kifo cha mtu fulani akasema hata kama Rwanda haijahusika lakini kwa nini watu hao waachwe ili waendelee na hujuma zao dhidi ya wananchi wasio na hatia? Na wengi ni wale aliowataja kama waliosahau kilicho watoa utumwani na sasa wanaigeukia nchi yao.

Kagame aliongeza na kusema "wale wanaosahau kilichowatoa utumwani, ni lazima wakabiliwe na athari ikiwa ni pamoja na hao mnaowasema, wamesahau wameshiba na kuvimbiwa kisha kusahau kilichowapa umaarufu huo, lakini kumbe wakasahau kwamba nchi yao Rwanda na Mungu aliyewaumba viko juu zaidi yao."

please wait

No media source currently available

0:00 0:02:32 0:00
Kiungo cha moja kwa moja

Rais Kagame ametoa tamko hili huku kukiendelea wimbi la lawama kupitia vyombo vya habari kwamba serikali ilikuwa na mkono kwenye mauaji ya mkuu wa zamani wa ujasusi nchini Rwanda Kanali Patrick Karegeya. Rais na serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha vikali kuhusika na mauaji hayo. Hata hivyo katika kuonyesha ukali wa shutuma zake dhidi ya wapinzani alitoa mfano.

Akisema "watu wanaokuja hapa na kurusha mabomu na kuua watoto wadogo wasio na hatia, polisi walioko wanafahamu vipande vya miili ya watu wanavyookota baada kuuawa na mabomu kisha uniambie niombe radhi?kamwe ."

Hii imekuwa mara ya kwanza kwa Rais Paul Kagame kutoa matamshi makali baada ya kuwepo na shutuma dhidi ya serikali kuhusu masaibu yanayowakabili wapinzani wa serikali katika nchi za kigeni.
XS
SM
MD
LG